MRADI WA KWEMBE MBIONI KUKAMILIKA WAFIKIA ASILIMIA 85

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) inaendelea kwa kasi na utekelezaji wa mradi wa maji katika Kata Kwembe wenye lengo la kuboresha huduma ya maji kwa wakazi zaidi ya 10,000 wa kata za Kwembe na Msigani.
Akielezea hatua za utekelezaji wa mradi huo, Meneja Mkoa wa DAWASA Kibamba Ndugu Erasto Emmanuel amesema hadi sasa kazi ya ulazaji wa bomba inafanyika usiku na mchana na tayari bomba zimelazwa la kwa umbali wa kilomita 3 kati ya kilomita 3.5 sawa na asilimia 85.
"Tunaendelea kuomba radhi kwa wateja wetu, tunaomba watuvumilie na tunategemea zoezi la kulaza mabomba na kuunganisha maji limalizike ndani ya Muda kama maelekezo ya Waziri wa Maji Mh. Jumaa Aweso" amesema Ndugu Emmanuel
Naye, Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa Malamba mawili Ndugu, Idd Mgweno ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mradi huu unaoenda kuwa mwarobaini wa changamoto ya maji katika mtaa wa Malamba mawili na mitaa jirani.
" Kwa kweli DAWASA hawajapoa ni utekelezaji tu hiyo inatia moyo kwamba jambo letu linakaribia kutimia, Tunawapongeza DAWASA nimejionea kasi ya utekelezaji ila swala ni moja tupate maji hivyo tunaomba mradi umalizike kwa wakati na wanachi wapate huduma" amesema Mwenyekiti Mgweno
Mradi wa maji Kwembe utanufaisha wakazi wa Kwembe, Kwembe Mpakani, King'azi A, King'azi B, Njeteni, Msigani, Malamba mawili, Baadhi ya maeneo ya Soweto na Kwa Hakimu.