Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MRADI WA MAJI BANGULO ULIVYOFUNGUA FURSA MPYA ZA BIASHARA KITUNDA
23 Oct, 2025
MRADI WA MAJI BANGULO ULIVYOFUNGUA FURSA MPYA ZA BIASHARA KITUNDA

Mradi wa Usambazaji Maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo) ambao umetekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), umeleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa Kitunda Relini, kata ya Kitunda, Wilaya ya Ilala. 

Kupitia mradi huu, wakazi sasa wanapata maji kwa uhakika, hali inayochochea kasi ya maendeleo ya biashara na kuboresha maisha yao.

Awali, wakazi wa Kitunda walikuwa wakitumia visima vya jumuiya ya watumia maji Kitunda na Makamba ambavyo havikuweza kukidhi mahitaji yao kutokana na uhitaji mkubwa uliosababishwa na ongezeko la watu pamoja na changamoto za usambazaji maji.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kitunda Relini, Ndugu Sospeter Marwa amesema ujio wa mradi wa maji Bangulo umebadilisha kabisa hali ya uchumi wa wakazi wa eneo hilo na kuwa chachu ya ukuaji wa maendeleo.

“Zamani wananchi waliteseka kutafuta maji, lakini sasa kila kaya inaunganishiwa huduma ya bomba, watu sasa wameanzisha biashara mpya kama kuosha magari, migahawa na saluni. DAWASA kwakweli imetuwezesha kujitegemea kiuchumi,” amesema Ndugu Marwa.

Miongoni mwa wajasiriamali wanaofaidika na mradi  ni Ndugu Godfrey Abdi anayemiliki kituo cha kuosha magari ambaye amesema kabla ya maji kufika, alilazimika kununua maji kwa bei kubwa kutoka kwa malori au kutumia maji ya kisima jambo lililopunguza faida. 

“Sasa maji yapo karibu, gharama zimepungua sana. Naosha magari, pikipiki pamoja na kufua mazuria. DAWASA imetusaidia sana kuinua kipato chetu,” amesema Ndugu Abdi.

Ndugu Mwanahawa Kombo, mfanyabiashara wa kuuza chakula katika eneo hilo amesema huduma ya majisafi imemrahisishia kufanya biashara kwa usafi na ufanisi zaidi hali ambayo imemuongezea wateja. 

“Kabla ya maji ya DAWASA, nilikuwa natumia muda mwingi kutafuta maji. Sasa napata maji kwa bomba, na wateja wangu wameongezeka kwa sababu usafi umeimarika,” amesema.

Kupitia mradi wa Bangulo, DAWASA imefanikiwa kuboresha maisha ya maelfu ya wakazi wa Kitunda Relini kwa kuwapatia huduma endelevu ya majisafi. Huduma hiyo imechangia katika uchumi wa wananchi kwa kufungua milango ya fursa mpya za biashara.