MRADI WA MAJI BANGULO UTACHOCHEA MAENDELEO, KUPUNGUZA GHARAMA ZA MAISHA

Viongozi wa Serikali za Mitaa Kata ya Pugu Station, Wilaya ya Ilala wamesema kukamilika kwa mradi wa usambazaji maji Dar es Salaam ya Kusini maarufu mradi wa maji Bangulo utachochea shughuli nyingi za maendeleo na italeta ahueni kubwa juu ya gharama za maisha kwa wananchi.
Mradi huo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 36 upo asilimia 99 ya utekelezaji wake chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA).
Viongozi hao wamesema hayo mara baada ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi huo sehemu linapojengwa tenki kubwa la kuhifadhi maji eneo la Bangulo hali ya hewa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Bangulo, Gudluck Mwele amesema baada ya mradi kuanza kufanya kazi shughuli nyingi za maendeleo zitafanyika vizuri mtaani kwake na italeta ahueni kubwa juu ya gharama za maisha kwa wananchi.
"Mradi huu ni msaada mkubwa kwetu, maeneo yetu haya tumekua tukinunua maji kwa bei kubwa sana lakini tunaona baada ya mradi kukamilika maji ya DAWASA yatakavyokua bei nafuu lakini zaidi kupatikana majumbani kwa wananchi," amesema Mwele.
Katibu wa CCM tawi la Bangulo, Tatu Kitungi amemshukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za mradi huu ambao unaenda kumaliza changamoto ya maji katika kata yao.
"Kama wasimamia Ilani, tunaona furaha kubwa mradi huu unapoenda kukamilika, fedha hizi zingeweza pelekwa pengine ila zikaletwa hapa kwetu.
Adha zote za ukosefu wa huduma ya maji na kufuata maji umbali mrefu sasa zinakwenda kumaliza na hapa niwapongeze DAWASA kwa usimamizi mzuri wa mradi huu," amesema Tatu.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi, Mhandisi John Romanus amesema kwasasa mradi huu unaogharimu Sh36 bilioni upo asilimia 99 ya utekelezaji wake na kukamilika kwake utahudumia wakazi zaidi ya 450,000 katika Kata za Mzinga, Kipunguni, Kitunda, Pugu station na Kiluvya huku kata za Msigani na Kinyerezi zikienda kuongezewa msukumo wa maji.