MRADI WA MAJI MSAKUZI - MACHIMBO HADI MAKABE WAFIKIA ASILIMIA 65, WANANCHI WAPONGEZA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea na kazi ya kuboresha hali ya upatikanaji huduma ya maji safi katika maeneo yake kihuduma kwa kutekeleza miradi mikubwa na midogo yenye tija kwa wananchi.
Moja ya miradi inayotekelezwa na Mamlaka kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji ni mradi wa uboreshaji huduma ya maji Msakuzi - Machimbo hadi Makabe ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 65.24
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Ubungo Mhandisi Damson Mponjoli amesema utekelezji wa mradi huo ni kutokana na maeneo hayo kuwa na changamoto kubwa sana ya maji kutokana na maeneo hayo kuwapo katika miinuko.
"Msakuzi-Machimbo hadi Makabe ni moja ya maeneo ambayo huduma ya maji ilikuwa kidogo changamoto na kutupelekea sisi kama DAWASA kuja na suluhu ya kuongeza mtandao wa maji kwa kulaza mabomba yatakayosaidia kuongeza msukumo wa maji kwa sababu maeneo haya yapo kwenye miinuko zaidi," amesema Mhandisi Mponjoli.
Mhandisi Mponjoli ameongeza kutokana na maeneo hayo kuwa na muinuko ndio imeifanya kuwepo na changamoto ya maji ila kwa sasa tatizo hilo linaenda kumalizika baada ya kazi hii kukamilika.
"Kukamilika kwa kazi hii ni imani yetu DAWASA kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa maeneo ya Msakuzi, Machimbo hadi Makabe na viunga vyake itaongezeka na kuimarika zaidi maana tunatambua maji ndio kila kitu na hata uchumi wa wakazi wa huku utakuwa zaidi," amesema Mhandisi Mponjoli.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Msakuzi, Ndugu Mariam Miraji Kiuko ameipongeza DAWASA kwa kazi kubwa ya kupambana usiku na mchana kuhakikisha changamoto ya maji iliyokuwa imedumu kwa muda mrefu inamalizika.
"Kiukweli niwe muwazi, sisi wakazi wa Msakuzi tulishakata tamaa ya kupata huduma ya maji ila kutokana na jitihada za DAWASA kuendelea kutuhakikishia tunaenda kupata maji sasa imani yetu kwao imerudi maana kazi tunaiona ulazaji wa bomba unavyoendelea na ukiangalia wapo asilimia 65 za utekelezaji kwa maana hatuna muda mrefu tunaanza kupata huduma ya maji safi, nawapongeza sana DAWASA kwa kazi kubwa," amesema Ndugu Mariam.
Aidha, Ndugu Samira Mohamed, mkazi wa Lubaba Msakuzi, Mtaa wa Baney ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan sambamba na DAWASA kwa kuondoa changamoto ya maji ambayo imekuwa ikigharimu sana ndoa na majukumu ya wakazi wengi wa Msakuzi na sasa imani na furaha ya wakazi imeanza kurejea baada ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo.
Mradi wa uboreshaji huduma ya maji Msakuzi - Machimbo hadi Makabe umefikia asilimia 65.24 ambapo unahusisha ulazaji wa bomba za inchi 8, 2 na inchi 1.5 kwa umbali wa kilomita 69.1 utakaonufanisha wakazi takribani 39,462 na kukamilika mapema ifikapo Juni 2026.
