WIZARA YA NISHATI NA MADINI ZANZIBAR YACHOTA UJUZI DAWASA
Wizara ya Maji Zanzibar yakagua miradi ya kimkakati ya Maji Dar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imepongeza kasi ya maendeleo ya miundombinu ya maji mkoani Dar es Salaam, huku ikieleza kuvutiwa na teknolojia ya kisasa ya uchimbaji wa visima virefu inayotumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Akizungumza leo, Jumapili Januari 18, 2026, mara baada ya kukagua mradi wa visima virefu vilivyopo Kimbiji, wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Nadir Abdullatif Alwardy, amesema ziara hiyo ina lengo la kujifunza na kuimarisha ushirikiano wa kisekta kati ya pande mbili za Muungano.
Waziri Alwardy, aliyeambatana na Naibu wake, Seif Kombo Pandu pamoja na Kamati ya Baraza la Wawakilishi, ameshuhudia uwekezaji mkubwa wa kisima hicho ikiwa ni moja wapo ya visima 11 ambavyo vimechimbwa kwa teknolojia ya hali ya juu.
“Tumejionea maendeleo na miundombinu ya kisasa kabisa ambapo leo tumeweza kushuhudia visima vikubwa sana ndani ya Tanzania vyenye takriban urefu wa mita 650 na kidogo chao basi takriban mita 400 ambavyo viko zaidi ya 11”, amesema Waziri Alwardy.
Waziri huyo amebainisha kuwa Wizara yake imeridhishwa na mifumo ya kisasa ya DAWASA na imejifunza mbinu mpya ambazo zitasaidia kuboresha upatikanaji wa maji visiwani Zanzibar. Aidha, ametoa mwaliko kwa watendaji wa DAWASA kutembelea Zanzibar ili kubadilishana uzoefu na kutoa ushauri wa kitaalamu katika miradi ya maji visiwani humo.
