Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MRADI WA MAJI SALASALA - LIVINGSTONE KUKWAMUA SHUGHULI ZA KIUCHUMI WAZO
20 Oct, 2025
MRADI WA MAJI SALASALA - LIVINGSTONE KUKWAMUA SHUGHULI ZA KIUCHUMI WAZO

Jumla ya wakazi 1,500 watanufaika na maboresho makubwa ya huduma ya maji  mtaa wa Salasala kata ya Wazo Wilaya ya Kinondoni.

Ni baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuanza utekelezaji wa mradi wa maji Salasala-Livingstone wenye lengo la kuongeza msukumo wa maji katika eneo hilo.

Mradi wa maji Salasala-Livingstone unaogharimu kiasi cha Shilingi Milioni 203 utahudumia maeneo ya Livingstone, Interchick, Wagiriki, Mbezi tiles, Mapanga Shaa, Luona, Salasala Magengeni , na Nabii Flora kwa kuwapatia huduma bora ya majisafi na endelevu wakati wote.

Akizungumza utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa DAWASA mkoa wa kihuduma Tegeta, Mhandisi Edson Robert amesema eneo la Salasala Magengeni na maeneo jirani yalikuwa yakipata maji kwa msukumo mdogo na kusababisha shughuli nyingi za wananchi kukwama jambo ambalo wamelipatia ufumbuzu kupitia mradi huu.

"Mradi huu unahusisha uchimbaji na ulazaji wa bomba lenye ukubwa wa inchi 6 kwa umbali wa kilomita 2.8 na kwa kiasi kikubwa utaimarisha sana huduma sio kwa wateja wa majumbani tu hata wale wakubwa wenye uhitaji wa maji mengi kwa siku huduma itaimarika sana," amesemaMhandisi Edson.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Salasala, Ndugu Robert Massawe ameipongeza DAWASA kwa usikivu na maamuzi ya haraka kuja na mradi huu ukizingatia wingi wa wakazi katika eneo hili na maeneo ya jirani.

"Eneo letu lina wingi wa wakazi na wanaongezeka kila siku, maji tuliyokuwa tunapata awali hayakukidhi mahitaji yetu, lakini sasa tumepata imani baada ya kuona kasi ya utekelezaji wa mradi huu ambao unakwenda kumaliza kabisa changamoto ya maji hapa mtaani kwetu na maeneo jirani na wananchi kunufaika na shughuli za kiuchumi zinazotegemea huduma ya maji kwa kiasi kikubwa," amesema Massawe.