Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MSUMI WAMIMINIKA KUOMBA HUDUMA YA MAJI
19 Feb, 2026
MSUMI WAMIMINIKA KUOMBA HUDUMA YA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), inaendelea na zoezi la upimaji tafiti na kuandikisha wateja wapya wa Mtaa wa Msumi, Kata ya Mbezi, Wilaya ya Ubungo wanaotarajia kunufaika na huduma ya majisafi baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa mradi wa maji Msumi. 

Mradi wa Maji Msumi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu na kunufaisha wakazi takribani 47,500 wa Msumi A, Msumi B na Msumi C pamoja na maeneo jirani.

Akizungumzia zoezi hilo, Mhandisi wa Miradi Mkoa wa Kihuduma DAWASA Ubungo, Mhandisi Sheka Mussa amesema zoezi hilo linaendelea vizuri kutokana na muitikio mkubwa wa wananchi baada ya utekelezwaji wa mradi wa maji Msumi ukiwa katika hatua za mwisho.

"Tunaendelea na zoezi la kuandikisha wananchi ambao wanakwenda kunufaika na huduma ya maji baada ya mradi huu kuelekea ukingoni. Ni matarajio yetu zoezi hili litafanikiwa kwa ukubwa zaidi ambapo hadi sasa tumeandikisha wakazi 1,560 na matarajio nikuunganishia wateja 47,000," amesema Mhandisi Sheka.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Msumi, Ndugu Jaqueline Juma ameipongeza DAWASA kwa kasi inayoendelea nayo kuandikisha wananchi ili kuhakikisha mwishoni mwa mwezi huu wanaanza kutumia huduma ya maji.

"Mtaa wangu una wakazi zaidi ya 40,000 tupongeza kazi kubwa inayoendelea kufanywa na DAWASA hasa ya kutuandikisha pamoja na kutufanyia vipimo ili kuhakikisha mwishoni mwa mwezi huu tunaanza kupata maji, hii ni hatua kubwa na tunafuraha kilio chetu kinakwenda kuisha," amesema Ndugu Jaqueline.

Mkazi wa Msumi, Ndugu Mwanaidi Hamis ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Jemedari Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na DAWASA kwa kutekeleza mradi mkubwa wa Msumi baada ya changamoto ya muda mrefu kwa wakazi wa Msumi ya kukosekana kwa huduma ya maji kwa miaka mingi.