MTENDAJI MKUU DAWASA AKAGUA HALI YA HUDUMA YA MAJI DAR NA PWANI

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) Mhandisi Mkama Bwire ametembelea mtambo wa kuzalisha maji Ruvu juu na kukagua hali ya uzalishaji na usambazaji maji.
Katika ziara hiyo Mhandisi Bwire amekagua pia matenki ya kuhifadhi maji Kibamba na Kimara ili kukagua ujazaji wa matenki hayo.
"Tunaendelea na jitihada nyingi kuboresha uzalishaji wa maji katika mtambo wetu wa Ruvu juu, jitihada ambazo tunaimani zitatupa majibu mazuri ya upatikanaji wa huduma kwa wateja wa maeneo ya Mbezi Luis, Kiluvya, Luguruni, Gogoni, Kibamba, Tabata, Kinyerezi, Saranga, Kitopeni na maeneo mengi ya jirani" ameelza Mhandisi Bwire.
Mhandisi Bwire ameongeza kuwa, maji ni haki ya kila mwananchi na Mamlaka haitachoka wala kupumzika mpaka pale itapohakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji.
Mhandisi Bwire amewahakikishia wananchi kuwa timu ya wataalamu ipo mtaani kuendelea kufatilia huduma ya maji katika maeneo mbalimbali na wateja wategemee kupata huduma.