Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MWENGE WA UHURU WAPONGEZA DAWASA UBORESHAJI HUDUMA ZA MAJI KIGAMBONI
15 Apr, 2026
MWENGE WA UHURU WAPONGEZA DAWASA UBORESHAJI HUDUMA ZA MAJI KIGAMBONI

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa , ndugu Michael Mwang'onda, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa utekelezaji mzuri wa mradi wa usambazaji maji katika Wilaya ya Kigamboni ulionufaisha Wakazi takribani 25,000 katika kata nne za  Kibada,Mjimwema,Vijinweni na Somangira Wilayani humo.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru kukagua miradi ya Maendeleo Wilayani Kigamboni akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa uendelezaji huduma za Maji Kizinza katika kata ya Kibada, ndugu Mwang’onda amesema kuwa maendeleo ya mradi yanaakisi dhamira ya dhati ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii zinazochochea maendeleo na ustawi wa jamii.

“Utekelezaji wa mradi huu unaendelea vizuri. Niipongeze Serikali kupitia DAWASA kwa kuhakikisha wananchi wanapata maji, mwenge wa Uhuru umeridhika na mradi huu, hivyo endeleeni kuwatumikia wananchi na kuongeza kasi ya kuwaunganishia huduma za Maji,” amesema ndugu Mwang’onda.

Kwa upande wake, Meneja wa DAWASA Kigamboni, ndugu Rashid Mpinzire, ametoa maelezo ya kina  kuhusu mradi huo akisema kuwa mradi wa Maji Kiziza umetokana  na utekelezaji wa awali wa mradi mkubwa wa Kigamboni uliotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 8.3. 

Amefafanua kuwa Mradi wa Maji Kizinza uliohusisha ulazaji wa mtandao wa  mabomba ya maji yenye kipenyo cha kuanzia inchi '3' mpaka '6' kwa urefu wa mtandao wa kilometa 62.

Ameongeza kuwa mradi huo umekamilika na unahudumia takribani wakazi 25,000 wa maeneo ya Kiziza katika kata ya Kibada ambao kwa muda mrefu walikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama. 

Pia ameeleza kuwa usanifu na utekelezaji wa mradi umezingatia viwango vya kitaalam ili kuhakikisha huduma inakuwa endelevu, yenye ufanisi na inayokidhi mahitaji ya sasa pamoja na ongezeko la baadaye.

Kwa ujumla, mradi huu ni sehemu ya juhudi mahsusi za Serikali katika kuimarisha huduma za maji na inatarajiwa kuboresha hali ya maisha ya wananchi, kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, na kuimarisha ustawi wa jamii katika Wilaya ya Kigamboni.