NAIBU KATIBU MKUU MAJI AHITIMISHA ZIARA DAWASA, ASISITIZA UWAJIBIKAJI KWA HUDUMA ENDELEVU
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Bi. Rose Zakaria Ambrose, amehitimisha ziara ya siku tatu katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na kusisitiza uwajibikaji na weledi katika utendaji kazi kwa kuhakikisha kila Mtumishi wa Sekta ya Maji anasimama vyema katika nafasi yake ili kuleta tija na ufanisi kwa Wizara na Mamlaka.
Amesisitiza uongozi wa DAWASA kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha Mwananchi anapata huduma ya Majisafi sambamba na kushughulikia changamoto za huduma kulingana na muda uliowekwa katika Mkataba wa huduma kwa Wateja (Customer Service Charter).
Katika ziara yake ndani ya eneo la kihuduma DAWASA, Naibu Katibu Mkuu alitembelea miradi ya Majisafi na usafi wa Mazingira inayoendelea kutekelezwa sambamba na mitambo mikubwa ya uzalishaji Maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini ambapo ameahidi Wizara ya Maji imepokea na itashughulikia changamoto mbalimbali za kisera zilizoainishwa.
