PAMPU MPYA ZAONGEZA MATUMAINI YA UHAKIKA WA HUDUMA UBUNGO
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)imeanza zoezi la ufungaji wa pampu mpya za kuzalisha maji katika Mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu kwa lengo la kuongeza kiwango cha maji yanayozalishwa kwenda kwa wateja hususani wa Jimbo la Ubungo.
Pampu hizo ambazo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza wigo wa upatikanaji mzuri wa huduma kwa wananchi, tayari zimewasili na kuanza kufungwa katika Mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu.
Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Albert Msando, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa Serikali imefanya kazi kubwa ya kutenga fedha kiasi cha Bilioni 16.5 kwa ajili ya ununuzi wa pampu mpya 8 zitakazosaidia kuongeza kiasi cha uzalishaji wa maji kwa wananchi.
Amebainisha kuwa tayari pampu 6 kati ya 8 zimeshawasili, na kazi ya kuzifunga imeanza katika Mtambo wa Ruvu Juu ambapo imeshafungwa moja na kazi inaendelea ya kufunga pampu 5 katika mtambo huu.
"Tumezipokea pampu hizi na kazi inaendelea ya kuzifunga, tunatarajia mpaka ifikapo mwisho wa mwezi huu wa sita tuwe tumemaliza kazi hii na kuziruhusu pampu ziweze kufanya kazi ya kutoa huduma ya maji kwa wakazi wengi hususani wa Jimbo la Ubungo, maeneo ya Msigani, Golani, Saranga na maeneo mengine," amesema Mhandisi Bwire.
"Zoezi hili linaenda sambamba na ukaguzi na ufuatiliaji wa miundombinu ya usambazaji wa maji kwenda kwa wananchi, kwa lengo la kubaini kama kuna sehemu yenye changamoto ya uvujaji itakayoathiri usambazaji ili izibitiwe kikamilifu," amesema Mhandisi Bwire.
Ameeleza kuwa pampu hizi zina uwezo mkubwa, ambapo pampu moja ina uwezo wa kuzalisha lita 1,500 za maji kwa siku, tofauti na pampu za sasa zenye uwezo wa kuzalisha lita 1,200 kwa siku. Hivyo zitaongeza upatikanaji wa maji kwa maji kwa wingi, na kuweza kukidhi mahitaji ya maji kwa wakazi wa Ubungo na maeneo mengine.
"Nipende kutanguliza Shukrani zetu za dhati kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuwezesha upatikanaji wa pampu hizi za maji zitakazosaidia kuongeza uzalishaji wa maji ili kuhudumia wananchi wengi zaidi," amesema Mhandisi Bwire.
Diwani Kata ya Msigani Ndugu Muliro Zaidi ameipongeza Serikali ya Mhe. Rais Dkt Samia kwa kufanikisha kupatikana kwa pampu hizi ambazo zinaleta matumaini kwa wananchi, tunatarajia shida ya maji maeneo ya Msigani itapungua kwa sasa.
