Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
RC CHALAMILA ATETA NA WATENDAJI DAR, AHIMIZA KASI YA HUDUMA ZA MAJI KUELEKEA AFCON 2027
16 Jun, 2026
RC CHALAMILA ATETA NA WATENDAJI DAR, AHIMIZA KASI YA HUDUMA ZA MAJI KUELEKEA AFCON 2027

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameielekeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuendelea kuimarisha huduma za maji safi na usafi wa mazingira ili kuhakikisha jiji linakuwa tayari kupokea wageni na washiriki wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha madiwani, wenyeviti wa mitaa, watendaji wa mitaa na wakuu wa wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam,Chalamila amesema huduma bora za maji na usafi wa mazingira ni miongoni mwa vigezo muhimu vitakavyoonyesha utayari wa Tanzania kuandaa mashindano hayo makubwa ya kimataifa.

Amesema pamoja na uwekezaji unaoendelea katika miundombinu mbalimbali, ni muhimu kuhakikisha wananchi na wageni watakaofika wanapata huduma za maji za uhakika na mazingira safi yatakayolinda afya za wananchi na wageni.

Chalamila ameipongeza DAWASA kwa ushirikiano wake mzuri na viongozi wa serikali za mitaa pamoja na madiwani katika kushughulikia changamoto za maji kwenye maeneo mbalimbali ya jiji, akieleza kuwa ushirikiano huo umechangia kupatikana kwa suluhisho la haraka kwa baadhi ya changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi.

“Ninaipongeza DAWASA kwa kufanya kazi kwa karibu na madiwani, wenyeviti na watendaji wa mitaa. Ushirikiano huu umeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kusaidia kutatua changamoto za wananchi kwa wakati,” amesema Chalamila.

Aidha, aliwataka viongozi hao kuendelea kuwa kiungo kati ya wananchi na  Dawasa kwa kutoa taarifa za changamoto zinazojitokeza kwenye maeneo yao ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa haraka na kwa manufaa ya wananchi.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA Mhandisi Mkama Bwire ameeleza kuwa Mamlaka inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira.

 "Tunaendelea na ufungaji wa pampu mpya za kusukuma maji ili kuongeza msukumo wa maji kwa wananchi, aidha DAWASA inaendelea na miradi ya majitaka katika maeneo ya Mbezi beach, Buguruni na maeneo  mengine ya pembezoni" amesema Mhandisi Bwire

Kwa kuimarika kwa huduma za maji na usafi wa mazingira, Dar es Salaam inatarajiwa kuwa katika nafasi nzuri ya kupokea wageni na washiriki wa AFCON 2027, huku wananchi wakinufaika na huduma bora zitakazoendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi hata baada ya mashindano hayo kumalizika.