RC CHALAMILA ATOA NONDO KWA WATENDAJI DAWASA KUBORESHA HUDUMA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila ametoa wito kwa Wafanyakazi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuzingatia nidhamu mahali pa kazi na kuwa na ushirikiano kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi wote wa Dar es Salaam.
Mhe. Chalamila ameyasema hayo wakati wa kikao cha Watumishi wa DAWASA cha kufunga na kufungua mwaka mpya wa fedha 2025/26 kilicholenga kutoa tathmini ya utendaji kazi kwa mwaka uliopita na kuweka bayana ya mikakati mipya kwa mwaka mpya wa fedha.
Amesema kuwa Watumishi wa Mamlaka wanatakiwa kuleta tumaini ya upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa kuwa Serikali imewekeza nguvu nyingi kwa Watumishi ili waweze kuwahudumia wananchi ipasavyo.
"Watumishi mnatakiwa kuwa na umiliki wa kazi yenu ya kutoa huduma kwa wananchi, kwa kufanya kazi kwa kuipenda ili kuleta tija kwa Taasisi na kuwezesha huduma ya majisafi iwe endelevu kwa wananchi kwa muda wote," amesema Mhe Chalamila.
Amewasisitiza watumishi kuwa na utii kwa Viongozi wao ili kuwezesha utendaji wa kazi kuwa bora na kuleta ufanisi katika kutoa huduma.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameipongeza Mamlaka chini ya uongozi wa Mhandisi Bwire kwa kuwa na bidii katika kutatua changamoto ya huduma ya majisafi kwa wananchi kwa wakati na kwa ufanisi.
"Mwaka mmoja wa Mhandisi Bwire umeleta mageuzi makubwa katika maboresho ya huduma ya majisafi katika maeneo mengi yaliyokuwa na changamoto ya maji, suluhu ya majisafi imepatikana," ameeleza Mhe. Mpogolo.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amewapongeza Watumishi kuwa utendaji wa kazi katika mwaka wa fedha uliopita na kuwataka kuongeza bidii zaidi ya kazi katika kuboresha utoaji wa huduma ili kukamilisha malengo yaliyopo.
Amesema kuwa yapo mafanikio yaliyopatikana ikiwemo ya kuongeza idadi ya wateja kupitia zoezi la maunganisho mapya ya maji yaliyofanyika kwa mwaka wa fedha uliopita.
"Kazi kubwa inatakiwa kufanyika kwa mwaka huu ikiwemo kuongeza nguvu katika kuzuia upotevu wa majisafi kwenye maeneo yote ya kihuduma ili kuokoa fedha zinazowekezwa kwenye usambazaji wa majisafi," amesema Mhandisi Bwire.
Amesisitiza kuwa kwa mwaka mpya wa fedha 2025/26 Watumishi kuiwezesha Taasisi kuwa suluhu ya changamoto ya maji kwa wananchi wa Dar es Salaam na Pwani.