Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
SARANGA WABORESHEWA HUDUMA, SASA MAJI NI MWA MWAA MWAA
15 Oct, 2025
SARANGA WABORESHEWA HUDUMA, SASA MAJI NI MWA MWAA MWAA

Viongozi waandamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wameendelea na zoezi la ufuatiliaji uimarikaji wa huduma ya Maji baada ya maboresho yaliyofanywa katika mfumo wa usambazaji maji.

Katika Wilaya ya Ilala, Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu, Mhandisi Lydia Ndibalema amesema kuwa kwa sasa huduma ya maji inaendelea kuimarika katika maeneo ya Saranga, Msitu wa Nyuki na Kisungu, hali iliyokuwa tofauti na hapo awali ambapo kulikuwa na changamoto za upatikanaji wa maji.

“Kwa sasa maji yanapatikana mara kwa mara, tunapokea maoni chanya kutoka kwa wateja wetu, hii ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na DAWASA kuhakikisha kila kaya inapokea huduma bora. Timu zetu ziko maeneo mbalimbali kuhakikisha huduma inaendelea kuimarika” alisema Mhandisi Ndibalema.

Mwenyekiti wa mtaa wa Saranga, Leonard Mbangile ameipongeza DAWASA kwa kuendesha zoezi la ufuatiliaji wa huduma ya maji pamoja na kupokea maoni ya wateja wao huku akitoa rai kwa DAWASA kuwafikia wateja wengi zaidi

"Zoezi hili ni tumaini kwa wananchi kwani DAWASA wameonesha kujali, kwa sasa huduma inaendelea kuimarika katika maeneo mbalimbali ndani ya mtaa wangu.Nitoe rai DAWASA kufikia wateja wengi zaidi ili kuhakikisha huduma inakuwa bora." amesema ndugu Mbangile