Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
SAUTI ZA MATUMAINI ZASIKIKA PANGANI, SERIKALI YATAJWA
22 Jul, 2025
SAUTI ZA MATUMAINI ZASIKIKA PANGANI, SERIKALI YATAJWA

Wananchi wanaonufaika na Mradi wa Maji Pangani- Kibaha wameipongeza Serikali kwa kuwatafutia suluhisho la tatizo la ukosefu wa maji lililodumu kwa kipindi kirefu katika maeneo yao. 

Sauti hizo za wananchi, wamezitoa takribani wiki moja kupita tangu Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuanza kufikisha miundombinu ya ujenzi kwenye eneo la mradi ikiwemo mabomba ya kusafirisha maji ya ukubwa wa inchi 6 yatakayolazwa kwa mita 1,100.

Mradi huo ulisainiwa mwaka 2023, unatarajia kuwanufaisha zaidi ya wananchi 14,868 wa maeneo ya ya Kibaha- Msufini, Lulanzi, TAMCO na Pangani, ukiwa na thamani ya Shilingi bilioni 9.8. 

Utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kusafirisha maji kiasi cha lita za ujazo wa milioni 5.2 kwa siku ambayo ni mahitaji ya miaka 20 ijayo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Pangani, Mwenyekiti wa Mtaa wa Pangani, Jitihada Hussein ametoa shukrani kwa Serikali kwa kusikia kilio chao cha maji na kuwaondolea changamoto ya kuyafuata maji mbali. 

"Tunaishukuru sana Serikali kwa kusikia kilio chetu cha muda mrefu na kutoa fedha za kutekeleza mradi huu, tuaona kazi imeanza na inatupa moyo kuwa sasa maji yataenda kupatikana muda wote," amesema Hussein. 

Ametoa wito kwa wananchi wa Kata yake kutoa ushirikiano katika maeneo ambapo mradi unakwenda kupita ili kuwezesha kazi hiyo iweze kutekelezwa kikamilifu na kwa wakati uliopangwa. 

Mkazi wa mtaa wa Mtakuja, Pili Maswali ametoa shukrani kwa Serikali kwa kuwakumbuka wanawake ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kwenda kufuata maji ya kutumia sambamba na lengo la Serikali la kumtua mama ndoo kichwani. 

"Mwanzo tulikuwa tunapata maji kupitia visima vifupi, tumefurahi mradi huu utakuwa mkombozi wa maendeleo yetu na shughuli za maendeleo zitaonekana sasa," amesema Pili. 

Ametoa ombi kuwa mradi utakapokamilika pawepo na usimamizi mzuri wa huduma ili maji yasiwe yanapatikana kwa wasiwasi kwa huko shida ya maji ni kubwa. 

Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Azizi Namanga amesema mradi huo unalenga kuhakikisha wakazi wa Kata ya Pangani wanapata huduma ya majisafi kwa muda wote. 

"Kazi kubwa ya ujenzi wa mradi ndo imeanza, hivyo tuwaombe wananchi wote kutoa ushirikiano wa ulinzi wa miundombinu ya maji kwa kuwa mradi huu unatekelezwa kwa manufaa yao na utakuwa kwao kwa muda wote," amesema Mhandisi Namanga.