SERIKALI KUTENGA BILIONI 400 KUIMARISHA USAFI WA MAZINGIRA DAR ES SALAAM NA PWANI

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) Mhandisi Mkama Bwire amebainisha kuwa Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 400 kuboresha huduma za Usafi wa Mazingira katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa Mwaka wa fedha 2024-2025 / 2025-2026 Ili kutekeleza miradi ya kimkakati itakayoleta tija kwa Wananchi zaidi ya milioni 5 katika mikoa hiyo.
Mhandisi Bwire ameyasema hayo katika mwendelezo wa vikao kazi na watumishi wa Idara ya Usafi wa mazingira wa Mamlaka kilicholenga kuangalia njia bora za kuboresha huduma hiyo kwa jamii.
"Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan kinakusudia kutenga fedha za miradi ya Usafi wa Mazingira kiasi cha Shilingi Bilion 400, hadi sasa ipo miradi mikubwa inayoendelea katika maeneo kama vile Mbezi beach, Buguruni, miradi ya ujenzi wa mitambo midogo ya kuchakata majitaka Kigamboni, mradi wa Majitaka Kurasini na miradi mingine mingi" ameeleza Mhandisi Bwire.
Mhandisi Bwire ameongeza kuwa kwa sasa kuna mabadiliko makubwa katika teknolojia ya idhibiti wa huduma za Usafi wa Mazingira, mabadiliko hayo yanayoka katika matumizi ya mabwawa ya kuchakata Majitaka hadi ujenzi wa mitambo mikubwa ya kuchakata majitaka. Hivyo Mamlaka itatoa kipaumbele katika mafunzo kwa Watumishi waendane na kasi hiyo ya Technolojia.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Usafi wa Mazingira, Mhandisi Lydia Ndibalema amewataka watumishi wa idara ya usafi wa mazingira kuwa na utayari wa kazi muda wote huku akibainisha matarajio ya kupokea vifaa mbalimbali vya utendaji kazi ifikapo Juni, 2025.
"Pamoja na changamoto katika usimamizi wa huduma ya Usafi wa Mazingira hususani kwa ongezeko la Watu, tumefurahi kusikia uwekezaji mkubwa utakaofanywa na Serikali ikiwemo ununuzi wa magari ya kuondosha majitaka pamoja na vifaa mbalimbali." ameeleza Mhandisi Ndibalema.