SERIKALI YACHUKUA HATUA KUBORESHA HUDUMA YA MAJI DAR

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amesema kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imechukua hatua za haraka za kuboresha huduma ya majisafi kwa Wananchi kwa kutoa fedha zaidi ya bilioni 6 za kununua mitambo ya kuzalisha majisafi ili kuimarisha upatikanaji mzuri wa huduma kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.
Mhe. Chalamila ameyasema hayo mara baada ya ziara ya kufuatilia hali ya upatikanaji wa maji kwa Wananchi wa Dar es Salaam na mikakati iliyopo ya kuimarisha huduma ya majisafi kwa wananchi.
Ameeleza kwa sasa changamoto iliyopo ya huduma ya Maji mjini inachangiwa na uchakavu wa mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu, inayosababisha huduma kupungua kutoka uzalishaji wa lita milioni 534 za maji kwa siku hadi lita milioni 520 kwa siku.
"Hivyo Serikali kwa kulitambua hilo, tayari imetoa fedha zaidi ya bilioni 6 kwa ajili ya kuagiza mitambo hiyo ya kuzalisha maji ambayo itaondoa changamoto ya maji na kuboresha huduma kwa wananchi walio wengi wa Dar es Salaam na Pwani," ameeleza Mhe Chalamila.
Ameongeza pia kuwa kazi nyingine itakayofanyia ni kufuatilia na kudhibiti upotevu wa maji kwenye maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam ambao unasababisha huduma kuwa hafifu kwa wateja, lakini kuikosesha Serikali mapato.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi kubwa ambayo imefanyika katika eneo la kihuduma DAWASA kwa uwekezaji mkubwa wa fedha nyingi za kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na pia kwa kuitikia na kuridhia kwa haraka suala la kuboresha miundombinu ya uzalishaji maji kwenye Mitambo kwa kutoa fedha za kununua mitambo hiyo.
Amesema pia kuwa Mamlaka itatekeleza agizo la kufanya tathmini ya hali ya huduma kwenye maeneo ya wananchi, sambamba na kudhibiti upotevu wa maji ili kuokoa kupoteza fedha za Serikali.