Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
SIKU TANO ZA DAWASA KUSAKA UJUZI ARUSHA
21 Aug, 2025
SIKU TANO ZA DAWASA KUSAKA UJUZI ARUSHA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imefunga safari kwenda Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Jiji la Arusha (AUWSA) kujifunza uzoefu wa uzalishaji na usambazaji maji hususan kupitia visima virefu pamoja na uendeshaji wake.

Watumishi wa DAWASA kutoka Idara ya Visima na Usambazaji Maji watakuwa huko kwa siku tano ambapo wamepokelewa na Menejimenti ya AUWSA na kisha kupata maelezo ya kitaalamu juu ya jinsi Arusha inavyotegemea na kuendesha miradi ya visima virefu kama chanzo kikuu cha maji kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa siku ya kwanza ya ziara hiyo, Kaimu Meneja wa Visima, Mhandisi Francisca Merere amesema ziara hiyo ni mwanzo wa ushirikiano mpana baina ya DAWASA na AUWSA katika kushirikiana kitaalamu, ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora, safi na salama ya maji.

"Tumekuja AUWSA kujifunza kutokana na uzoefu wao mkubwa katika kuendesha miradi ya visima. Dar es Salaam tuna mradi wa Kigamboni unaotegemea maji kupitia visima virefu hivyo tunahitaji mbinu bora zaidi za kuongeza uzalishaji na usimamizi wa miradi ya visima. Tunashukuru kwa ukarimu na ushirikiano kutoka AUWSA," amesema. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira kutoka AUWSA, Mhandisi Upendo Shushu amesema ziara hiyo ni fursa ya kubadilishana uzoefu kwani wote ni watoa huduma za maji kwa wananchi.

"AUWSA tumefurahi kuwapokea wenzetu kutoka DAWASA. Tumewaonesha jinsi tunavyosimamia miradi ya visima kwa kutumia teknolojia na mifumo ya ufuatiliaji ili kuhakikisha wananchi wa Arusha wanapata huduma ya maji kwa uhakika.

Tunaamini uzoefu tuliobadilishana leo utasaidia kuboresha huduma Dar es Salaam na pia kuongeza mshikamano kati ya mamlaka zetu," amesema Ndugu Shushu. 

Mbali na kujifunza mbinu za kiufundi, ziara hiyo pia imelenga kubadilishana mikakati ya kudhibiti upotevu wa maji, kuhakikisha ubora wa huduma kwa wateja na kulinda vyanzo vya maji ili huduma ibaki endelevu.