Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
SPIKA ZUNGU AIPONGEZA DAWASA KUCHIMBA VISIMA ILALA
20 Feb, 2026
SPIKA ZUNGU AIPONGEZA DAWASA KUCHIMBA VISIMA ILALA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea na utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso ya kuongeza vyanzo vya upatikanaji wa maji kwa uchimbaji wa visima virefu vya maji vitakavyo uunganishwa katika mtandao wa Mamlaka.

Lengo ni kusaidia utoaji wa huduma ya majisafi kwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Akizungumza katika ziara ya kukagua kazi ya majaribio ya kisima cha maji Mchikichini kilichopo Wilaya ya Ilala, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mheshimiwa Mussa Zungu (Mb) ameipongeza DAWASA kwa utekelezaji wa uchimbaji wa kisima hicho.

"Kisima hiki cha Ilala Mchikichini ni kati ya visima vitano vinavyotekelezwa na DAWASA ikiwemo vya Shariff Shamba, Garden, Ilala kata na Kariakoo ambapo katika kisima hiki kina uwezo wa kuzalisha maji lita za ujazo laki tatu na siku," amesema Mheshimiwa Zungu.

Kwa upande wa DAWASA, Afisa Msimamizi wa Visima, Mhandisi Iddi Nassor amesema uchimbaji wa visima vitano umekamilika na kazi kubwa ni kufanya majaribio ya kupata uwezo wa uzalishaji wa visima hivyo kwa siku.

"Kisima cha maji Mchikichini tayari kimekamilika na hatua ya leo Mheshimiwa Mbunge amefika kukagua ni zoezi la majaribio ya kupata uwezo wa uzalishaji wa kisima ambapo kinatarajia kuhudumia wakazi takribani 18,000 wa mtaa wa Mchikichini na maeneo ya jirani,” amesema Mhandisi Iddi.

Mamlaka katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji inaendelea kukamilisha uchimaji wa visima vya maji katika maeneo mbalimbali ikiwemo, uchimbaji wa visima 11 katika mtambo wa uzalishaji Ruvu chini wilayani Bagamoyo na kisima kimoja eneo la Kivule Sokoni.