Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
SULUHU YA MAJI MBANDE YAPATIKANA, WAKAZI 600 KUNUFAIKA
15 Oct, 2025
SULUHU YA MAJI MBANDE YAPATIKANA, WAKAZI 600 KUNUFAIKA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inatekeleza mradi mpya wa huduma ya maji kwa wakazi wa Kata ya  Chamanzi, mtaa wa Mbande, Wilaya ya Temeke.

Mradi huo umehusisha ulazaji wa bomba za inchi 6, 4 hadi mbomba la kipenyo cha inchi 2, bomba za inchi 6 imetoka kwenye bomba la kipenyo cha inchi 10.

Mradi una umbali wa kilomita 5.2. Kukamilika kwa mradi huu kutanufaisha wakazi takribani 600  lengo ni kumaliza tatizo la maji kwa wakazi hao.

Akizungumzia mradi huo, Meneja wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Mbagala, Ndugu Julieth John  amesema utekelezji wa mradi huo unafanyika kutokana na maeneo hayo kutokuwa na huduma ya maji na kusababisha usumbufu wa upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama.

"Kisewe na Mbande Magengeni ni moja ya maeneo ambayo huduma ya maji ilikuwa haijafika na kupelekea sisi kama DAWASA kutafuta suluhisho la changamoto inayowakabili wananchi wa eneo hili," amesema Ndugu Julieth

Naye Mhandisi Emmanuel Huja amesema, kutokana na maeneo hayo kuwa na ukosefu wa huduma ya maji  kwa muda mrefu, kumesababisha kuwepo kwa changamoto ya maji ila kwa sasa tatizo hilo linakwenda kumalizika baada ya kazi hii kukamilika.

"Kukamilika kwa kazi hii kutaboresha na kuimarisha huduma ya maji katika maeneo haya maana tunatambua maji ndio kila kitu na sasa adha iliyokuwa mwanzo inakwenda kuisha kwani tuko hatua za mwisho kukamilisha," amesema Mhandisi Huja.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbande, Ndugu Adam Nikolo  ameishukuru na kuipongeza DAWASA kwa hatua kubwa iliyochukuwa ya  kuondoa changamoto ya maji iliyokuwa imedumu kwa muda mrefu.

"Mimi kama kiongozi wa mtaa huu nakiri tumekuwa na shida ya maji kwa kipindi kirefu na baada ya kupata taarifa ya mradi huu naona tunakwenda kusahau kabisa tatizo hili.

"Nipende kuishukuru DAWASA kwa niaba ya wananchi wangu kwa kutukumbuka na kutusogezea  huduma karibu maana tulikuwa tunapata shida sana," amesema Ndugu Adam Nikole.

Ndugu Ally Juma, mkazi wa Kisewe  ameipongeza DAWASA kwa kuwasogezea huduma ya maji karibu inayokwenda kuondoa  changamoto ya maji  iliyowatesa kwa muda mrefu, ameiahidi DAWASA kuwa mjumbe wa kuhamasisha utunzaji wa miundo maji katika eneo lao.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira DAWASA inafanya kazi kwa bidii kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya majisafi na salama kwa ustawi wa jamii.