TUSHIRIKISHE JAMII KUTUNZA UPOTEVU WA MAJI

Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazigira Dar es Salaam (DAWASA) Mlandizi, wamepewa mbinu za namna bora ya kuishirikisha jamii katika kupunguza upotevu wa maji ili kuhakikisha rasilimali za maji zinatunzwa kwa manufaa ya wote.
Mbinu hizo zimetolewa ili kuwawezesha kuwasiliana na kushirikiana kwa karibu na wananchi ili kuibua uelewa na uwajibikaji wa pamoja katika kulinda miundombinu ya maji.
Kupitia mafunzo hayo, watumishi wamehamasishwa kushirikiana na wananchi katika kuripoti uvujaji wa mabomba, matumizi sahihi ya maji na kuhimiza matunzo ya vyanzo vya maji.
Akitoa elimu hiyo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa DAWASA, Ndugu Peter Shirima amesema Mamlaka inaamini ushirikiano wa jamii na taasisi ni nguzo muhimu katika kupunguza upotevu wa maji na kuhakikisha huduma endelevu kwa vizazi vijavyo.
"Kudhibiti upotevu wa maji inawezekana, kwa kuanzia kwetu sisi watumishi na kwa kushirikisha na jamii juu ya athari zitokanazo na upotevu wa maji," amesema Ndugu Peter.
Mmoja wa watumishi waliopata mafunzo, Ndugu Pascal Akaombwe amesema mafunzo haya ni ya muhimu kwa kuwa yanawajengea uzoefu wa namna ya kushirikisha jamii ikiwemo viongozi na wananchi ili kupunguza upotevu wa maji kwa pamoja.
"Tumekumbushwa uwajibikaji na kufanyakazi zetu kwa ufanisi, tukifanikiwa katika hili na jamii yetu ikaelewa zaidi athari za mivujo miundombinu yetu itaweza kukaa kwa muda mrefu zaidi," amesema Ndugu Akaombwe.