UBORESHAJI HUDUMA ZA USAFI WA MAZINGIRA ZAWAKUTANISHA WADAU MKOANI DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imewakutanisha wadau wa Usafi wa Mazingira wakiwemo Maafisa Afya wa Halmashauri, Wenyeviti wa Mitaa, Watoa huduma binafsi na wadau wa asasi za kiraia kwa lengo la kujadili namna ya kuboresha huduma za usafi wa mazingira kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea katika Mkoa wa Dar es salaam.
Akizungumza wakati wa warsha hiyo , Msimamizi wa Miradi ya usafi wa Mazingira DAWASA, Mhandisi Amon Gracephord amesema DAWASA inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kuboresha huduma ya usafi wa mazingira kupitia ikiwemo ujenzi wa mitambo ya kisasa ya kuchakata takatope, ujenzi wa mifumo rahisi ya uondoshaji majitaka katika makazi ya watu, ujenzi wa vyoo vya umma pamoja na ununuzi wa magari ya kisasa ya kuondosha majitaka.
"Pamoja na miradi inayoendelea kutekelezwa, Mamlaka tunajivunia ukamilishwaji wa ujenzi wa vyoo 30 vya umma ambavyo vitakuwa mkombozi katika maeneo yenye mkusanyiko vilivyojengwa katika halmashauri zote tano. Kupitia warsha hii itatusaidia kuboresha ushirikiano kati yetu na wadau muhimu na kusaidia kuboresha huduma ya Usafi wa Mazingira" amesema.
Dr. Sibomana Leonard, mbobezi wa huduma za Usafi za Mazingira kutoka kwa mkandarasi mshauri kampuni ya Economic and Basic Foundation(EBF) amesema wanafanya kazi kwa karibu na DAWASA ili kusaidia kujenga uelewa juu ya huduma za usafi wa mazingira pamoja na kuchochea mabadiliko ya tabia miongoni mwa wanufaika wa miradi hii.
Warsha hii ni muendelezo wa juhudi za Mamlaka za kujenga mahusiano mazuri na wadau katika utoaji wa huduma ya Majisafi pamoja na huduma ya usafi wa mazingira.