Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
UJENZI BWAWA LA KIDUNDA WAFIKIA ASILIMIA 40, KUKABILI MABADILIKO YA TABIANCHI
17 Dec, 2025
UJENZI BWAWA LA KIDUNDA WAFIKIA ASILIMIA 40, KUKABILI MABADILIKO YA TABIANCHI

Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mb) amesema kukamilika kwa ujenzi wa Bwawa la Maji Kidunda kutasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwemo ukame wa muda mrefu utakaomaliza tatizo la maji jijini Dar es Salaam.

Aweso amesema hayo leo Jumanne, tarehe 16 Desemba mwaka huu katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwala hilo uliofikia asilimia 40 akiambatana na Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Albert Chalamila, Abubakar Kunenge wa Pwani na Adam Malima wa Morogoro ambayo itanufaika na mradi huo.

"Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha zaidi ya Shilingi Bilioni 335 kutekeleza mradi huu wa kimkakati ambao kukamilika kwake kutamaliza changamoto ya upatikanaji wa maji hususani kipindi cha ukame," amesema Mheshimiwa Aweso. 

Amewaomba wananchi kulinda vyanzo vya maji lakini pia kuwa na utaribu mzuri wa kuhifadhi maji wakati Serikali inaendelea kuboresha hali ya upatikanaji huduma ya maji nchini kote.

Aidha, Mheshimiwa Aweso amesema Serikali katika kutatua changamoto ya maji nchini kote imeanza utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji kwa kuunganisha vyanzo vya maji vyote vikubwa nchini ili wananchi wapate huduma.

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Adam Malima amesema swala la utunzaji wa vyanzo vya maji lazima lichukuliwe kwa umuhimu wa hali ya juu na kwa ushirikiano wa mikoa yote mitatu ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro watahakikisha mto unabaki salama na kutumiwa kwa matumizi sahihi pekee.