UJENZI TANKI KUBWA LA MAJI MSUMI WAANZA, DAWASA YAPONGEZWA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 500,000 katika eneo la Msumi, Wilaya ya Ubungo, kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi takribani 22,370.
Mradi huo unaotekelezwa kwa fedha za ndani za DAWASA unagharimu Shilingi milioni 996 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Aziz Namanga, amesema ujenzi ulianza Mei mwaka huu na ni sehemu ya jitihada za DAWASA za kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika eneo la Msumi.
“Tumekusudia kuondoa kabisa malalamiko ya ukosefu wa maji katika eneo hili. Kwa sasa tupo katika hatua ya ujenzi wa msingi wa tanki na tunahakikisha kazi zote zinakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma ya maji kwa uhakika,” amesema Mhandisi Namanga.
Amefafanua kuwa mradi huo utatekelezwa kwa hatua tatu ambazo ni ujenzi wa msingi, usimikaji wa nguzo na ujenzi wa tanki pamoja na kufunga mabomba ya kuingiza na kusambaza maji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Msumi, Bi. Jacqueline Juma, ameipongeza DAWASA kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maji inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
“Ujenzi wa tanki hili ni matumaini makubwa kwa wakazi wa Msumi. Tunaamini utakuwa suluhisho la kudumu la changamoto ya maji ambayo imekuwa ikiwakabili wananchi kwa muda mrefu. Tunawashukuru DAWASA kwa jitihada hizi,” amesema.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Oktoba 2026 na utaongeza uwezo wa kuhifadhi na kusambaza maji katika maeneo ya Msumi A, Msumi B, Msumi C na Tegeta A. Tanki hilo litakuwa likipokea maji kutoka kituo cha kusukuma maji cha Msumi, hatua inayotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wakazi wa maeneo hayo.
