UJENZI WA TANKI KUBWA LA MAJI MSUMI WAINGIA HATUA YA MSINGI, DAWASA YAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA
Ujenzi wa tanki kubwa la kuhifadhi maji litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi lita 500,000 katika eneo la Msumi, Wilaya ya Ubungo, umeingia hatua muhimu ya ujenzi wa msingi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) za kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wapatao 22,370.
Mradi huo unaotekelezwa kwa kutumia fedha za ndani za DAWASA kwa gharama ya Shilingi milioni 996, unatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba na kuwa suluhisho la kudumu la changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya Msumi na viunga vyake.
Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Aziz Namanga, amesema kuwa kazi zinaendelea kwa kasi katika hatua ya ujenzi wa msingi wa tanki, ambapo maandalizi hayo ndiyo yatakayoweka msingi imara wa miundombinu hiyo muhimu.
"Kwa sasa tunaendelea na ujenzi wa msingi wa tanki. Hii ni hatua muhimu inayohakikisha tanki linakuwa imara na salama kwa matumizi ya muda mrefu. Lengo letu ni kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma ya maji ya uhakika," amesema Mhandisi Namanga.
Ameeleza kuwa baada ya kukamilika kwa msingi, ujenzi utaendelea kwa usimikaji wa nguzo, ujenzi wa tanki lenyewe pamoja na ufungaji wa mabomba ya kuingiza na kusambaza maji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Msumi, Bi. Jacqueline Juma, amepongeza DAWASA kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo, akisema unatoa matumaini mapya kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji.
"Tunafurahi kuona ujenzi unaendelea vizuri. Mradi huu utaleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa Msumi na maeneo jirani. Tunaishukuru DAWASA kwa kuendelea kuwekeza katika huduma muhimu zinazogusa maisha ya wananchi," amesema.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Oktoba 2026, ambapo tanki hilo litakuwa likipokea maji kutoka Kituo cha Kusukuma Maji cha Msumi na kuongeza uwezo wa kuhifadhi pamoja na kusambaza maji katika maeneo ya Msumi A, Msumi B, Msumi C na Tegeta A, hatua itakayoboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi, salama na ya uhakika kwa maelfu ya wakazi wa maeneo hayo.
