UPUNGUFU WA MAJI MTONI NI KUTOKANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI - WAZIRI MKUU DKT. NCHEMBA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mwigulu Nchemba amesema kuwa changamoto ya maji iliyotokea hivi karibuni siyo uzembe wa mtu bali ni kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri nchi yoyote.
Amesema kuwa mabadiliko ya tabianchi ni jambo mtambuka linaloikumba nchi yoyote Duniani, na imekuwa ikileta athari mbalimbali ikiwemo ukame kama ilivyotokea hapa.
"Pamoja na changamoto hii nipende kuwajulisha wananchi kuwa Serikali haijalala na imeliona suala hili na tayari hatua madhubuti za kukabiliana na hali hii kwa kipindi kijacho zilishachukuliwa ili kuepusha kutokea kwa changamoto ya namna hii," amesema Mhe. Nchemba alipokuwa kwenye ziara ya kukagua hali ya maji katika Mtambo wa Ruvu Chini.
Hatua hizo ni pamoja na ujenzi wa mradi wa kisasa wa Bwawa la Kidunda lenye uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 195 za maji zitakazotumika kwa kipindi chote cha ukame.
Mhe. Dkt. Nchemba ameongeza kuwa Serikali imeongeza nguvu katika matumizi ya vyanzo vya maji ya ardhini ikiwemo visima virefu vilivyochimbwa Kigamboni, ambavyo vilisaidia kukuza upatikanaji wa maji, na pia tunakusudia kuongeza wigo wa vyanzo hivyo ili viweze kutoa huduma kwa ukubwa.
"Niwahakikishie wananchi kazi iliyofanyika katika Mto Ruvu na kwenye Mtambo wa Ruvu Chini ya kufuatilia maji ni kazi makini na imesaidia kwa kiasi kikubwa maji kurejea Mtoni, hivyo niwatoe hofu wananchi hali ya maji kwa sasa iko salama," amesema Mhe. Nchemba.
Kwa upande wake Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ameishukuru Serikali kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi wa visima Kimbiji ambao umesaidia kutoa maji ya visima na kulisha wakazi wa maeneo ya katikati mwa Jiji.
Pia niwapongeze sana Watumishi, Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya DAWASA kwa kujitoa kwao kwa kipindi chote cha changamoto hii.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema kupungua kwa maji Mtoni kunatokana na mabadiliko ya hali ya hewa, yaliyosababisha mvua za masika kuchelewa kunyesha, pamoja na matumizi ya Mto kuzidiwa.
"Hivyo DAWASA kwa kushirikiana na Wizara na Bonde la Wami tulifanya doria ili kuondoa wakulima katika Mto, lakini pia tulitumia vyanzo vya maji ya visima vya Kigamboni vilivyosaidia kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi wa kati ya mji," ameeleza Mhandisi Bwire.
Mpango uliopo wa DAWASA kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, ni kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa visima Kimbiji - Mpera ili kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi.
