Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
USAJILI MAGARI YA UONDOSHAJI MAJITAKA WAANZA RASMI, WATOA HUDUMA WAITWA
28 Jan, 2026
USAJILI MAGARI YA UONDOSHAJI MAJITAKA WAANZA RASMI, WATOA HUDUMA WAITWA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza rasmi zoezi la kawaida la usajili na utoaji wa vibali kwa watoa huduma ya uondoshaji majitaka kupitia magari jijini Dar es Salaam kwa mwaka 2025-2026.

Zoezi hili la utambuzi, usajili na utoaji wa vibali litafanyika kwa muda wa wiki mbili kwanzia tarehe 26.1.2026 hadi tarehe 8.2.2026 katika mabwawa ya kuchakata majitaka Kurasini.

Akizungumzia zoezi hilo, Afisa Biashara Idara ya Usafi wa Mazingira DAWASA, Ndugu Coleta Msaghaa amesema ni muhimu kuwatambua watoa huduma na kuwapatia vibali kwa kuwasajili.

"Tunawasajili watoa huduma hawa ili tuweze kuwatambua na kuwapa vibali, hili litatusaidia kuwafanya waweze kumwaga majitaka katika maeneo rasmi yanayotambulika na kusaidia kuepuka uchafuzi wa mazingira kwa kumwaga majitaka kiholela," amesema Msaghaa.

Msaghaa amesema mmiliki wa gari anapofika kusajiliwa afike na nyaraka kama vile kopi ya kadi ya usajili wa gari, kopi ya fomu/cheti cha ukaguzi wa uzito na vipimo, kopi ya leseni ya dereva anayeendesha chombo husika, kopi ya kitambulisho cha NIDA ya mmiliki wa gari na namba ya leseni ya biashara (TIN number) ili kukamilisha usajili wa gari lake.

Kwa upande wake, mmoja wa madereva wanaotoa huduma ya kuondosha majitaka, Ndugu Michael Eliud amewaasa wamiliki na madereva wengine waweze kufika katika mabwawa ya majitaka Kurasini kusajili magari yao na kufanya kazi zao kihalali.

"Zoezi hili ni la muda mfupi sana, tujitokeze kwa wingi tuweze kusajiliwa magari ili tutambulike na Mamlaka husika na kufanya kazi zetu kwa uhuru na sio tu wamiliki wa magari binafsi tu zoezi hili ni mpaka kwa makampuni yanayomiliki magari ya uondoshaji majitaka tufike na kusajiliwa Ili tutambulike," amesema Ndugu Michael.