Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
USAJILI WATOA HUDUMA ZA MAJITAKA WAANZA
24 Jun, 2024
USAJILI WATOA HUDUMA ZA MAJITAKA WAANZA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza zoezi la usajili kwa watoa huduma binafsi na utoaji vibali vya uendeshaji wa magari yanayotoa huduma za Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (faecal sludge Emptiers) linaloendelea katika eneo la mabwawa ya majitaka Vingunguti, Dar es Salaam. 

Zoezi hilo limeabza tarehe 18-25, Juni 2024 kwa lengo la kuhakikisha inawatambua  watoa huduma kwa kuwasajili kama ilivyo katika muongozo wa Mdhibiti wa huduma za Nishati na Maji (EWURA)

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Biashara bi, Rogathe Minja amesema zoezi hilo hufanyika mara moja Mwaka kwa kushirikiana na watoa huduma binafsi kwa lengo la kupata takwimu na kuwafahamu, kuwafuatilia kwa karibu wanapotoa huduma katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.  
Amebainisha kuwa magari yote yatakayopata vibali vya uendeshaji wa huduma yatabandikwa stika maalum za DAWASA.

"Tumeanza usajili na tunatarajia kuendesha zoezi hili ndani ya siku saba za kazi, na baadae zoezi litaendelea katika ofisi zetu kwa muda wa mwezi mmoja. Zoezi hili litasaidia kuboresha huduma ya Usafi wa Mazingira kwa kuhakikisha majitaka yanamwagwa katika maeneo maalum yanayotambuliwa na DAWASA." amesema. 

"Baada ya muda wa usajili kuisha, yeyote atakayekutwa anatoa huduma ya uondoshaji na usafirishaji Majitaka katika eneo la huduma la DAWASA bila kibali hai cha uendeshaji atachukuliwa hatua kali za kisheria"aliongezea

Mmoja wa wamiliki wa magari ya majitaka, ndugu Ramadhani Abdallah amewapongeza DAWASA kwa zoezi la usajili na kusisitiza kuwa linawasaidia kwa kiasi kikubwa kutambulika na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.

"Tumekuwa tukishirikiana na DAWASA kwenye maeneo ya shughuli zao hivyo kwa zoezi hilo la usajili litaweza kusaidia kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza ikiwa hatujajisajili." ameeleza.