VIONGOZI UBUNGO WARIDHISHWA NA UWAJIBIKAJI DAWASA

Waungana kupongeza jitihada za uboreshaji wa huduma
Viongozi wa Wilaya, kata na mitaa ya Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo wameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa utendaji kazi bora pamoja na namna wanavyoshirikiana na viongozi wa Wananchi katika kutatua na kujenga mashirikiano baina yao.
Hayo yameelezwa wakati wa kikao kazi cha DAWASA na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kilichoongozwa na Naibu Meya wa Manispaa ya Ubungo, Mhe. Yusuph Yenga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya Ubungo, Wawakilishi wa Chama Tawala Wilaya, Madiwani wa kata 14 pamoja na Wenyeviti wa Mitaa 90 kutoka ndani ya Wilaya ya Ubungo.
Naibu Meya wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Yusuph Yenga ameipongeza DAWASA kwa kuwashirikisha viongozi katika utekelezaji wa shughuli za Mamlaka ndani ya kata na mitaa ndani ya wilaya ya Ubungo.
"Sisi kama viongozi tunapata matumaini na imani kubwa kwa DAWASA haswa baada ya kushirikishwa katika mikakati ya uboreshaji wa huduma za Maji, tunaishukuru DAWASA kwa kutujengea uwezo naamini wenyeviti watakwenda kuwa mabalozi wazuri na kuisemea DAWASA kwa Wananchi" amesema.
Mhe. Yenga ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wenyeviti kuisaidia Mamlaka kufikia malengo yake ikiwemo kuzuia ujenzi holela wa makazi ambao unachangia uharibifu wa miundombinu pamoja na kuchochea upotevu wa maji hivyo kuisababishia Mamlaka hasara.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema DAWASA imejipanga kuboresha huduma katika mitaa yote 90 kupitia mipango ya muda mrefu na muda mfupi.
"Kwa sasa tuko katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo mradi wa usambazaji maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo), Manunuzi ya pampu katika mitambo ya uzalishaji maji pamoja na miradi midogo midogo ya usambazaji maji katika wilaya ya Ubungo."ameeleza
Mhandisi Bwire ametoa rai kwa viongozi kuwa wa kwanza katika kuwasilisha changamoto zinazoibuka katika mitaa ili zifanyiwe kazi haraka na kwa ubora.
Viongozi wa Ubungo walipata fursa ya kutembelea mtambo wa uzalishaji maji Ruvu Juu pamoja na kujiona maendeleo ya ujenzi wa mtambo wa kisasa wa kuchakata takatope katika eneo la Kisopwa utakaokuwa na uwezo wa kuchakata lita 170,000 kwa siku.