Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
WAKAZI 3,500 WA MLANDIZI WABORESHEWA HUDUMA YA MAJI
14 Nov, 2025
WAKAZI 3,500 WA MLANDIZI WABORESHEWA HUDUMA YA MAJI

Takribani wakazi 3,500 wa Kata ya Mihande, vitongoji vya Mihande na Kibwende katika mji wa Mlandizi, Mkoa wa Pwani wanatarajiwa kunufaika na huduma ya majisafi kupitia utekelezaji wa mradi wa maji Mihande unaoendelea kutekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA). 

Mradi huu umeanza kutekelezwa hivi karibuni ukiwa na lengo la kuboresha huduma ya maji na kuwafikia wananchi wengi zaidi pamoja na taasisi zilizokuwa na changamoto ya upatikanaji wa majisafi. 

Mradi huo ambao utakuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa eneo hilo, unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi, Mhandisi wa miradi wa DAWASA Mlandizi, Ally Migeyo amesema mradi unatekelezwa kwa umbali wa kilomita 9.1 utatekelezwa katika awamu mbili, lakini baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza wananchi wataanza kupata huduma ya maji. 

"Awamu ya kwanza ya mradi inatekelezwa kwa umbali wa kilomita 3.5 ambapo kazi ya uchimbaji inaelekea kukamilika na kazi ya ulazaji wa bomba za inchi 3 za kusambaza maji kwa wananchi inaendelea," ameeleza Mhandisi Migeyo. 

Ameongeza baada ya kukamilika kwa maboresho hayo, wanatarajia kuongeza wateja zaidi ya 300 kutokana na mradi huo, kwa kusogeza zaidi huduma ya maji kwa wananchi. 

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mihande, Ndugu Teddy Mwaiswelo amesema furaha yake kwa Mamlaka kwa namna ambavyo hawajasahaulika kwa kutafutiwa ufumbuzi wa tatizo la huduma ya maji kwa muda mrefu. 

"Nipo tayari kushirikiana na DAWASA ili kazi hii ikamilike kwa wakati na kuendelea kuhamasisha wananchi katika Kitongoji hiki kutoa ushirikiano pindi utakapohitajika ili tuwe wa kwanza kupata huduma hii muhimu," ameeleza Ndugu Teddy.

Kwa upande wake, Natujwa Juma, mkazi wa Mihande amesema jitihada za utekelezaji wa mradi huu zinaleta matumaini ya kuwepo kwa maji ya uhakika na ya kutosha.