Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
WAKAZI 68,000 ZINGIZIWA NA CHANIKA KUNUFAIKA NA HUDUMA YA MAJI
21 Aug, 2025
WAKAZI 68,000 ZINGIZIWA NA CHANIKA KUNUFAIKA NA HUDUMA YA MAJI

Wakazi wa maeneo ya Zingiziwa, Msongola na Chanika, Wilaya ya Ilala wana matumaini ya kuanza kupata huduma ya maji, baada kukamilika kwa zoezi la upimaji wa wingi wa maji katika kisima cha maji kilichochimbwa katika ofisi ya kata ya Zingiziwa.

Kisima hicho kilichopo mtaa wa Ngobedi, kata ya Zingiziwa Wilaya ya Ilala kinatarajiwa kuzalisha takribani lita milioni 4.8 kwa siku, kwa hatua hii inayotajwa ni mkombozi kwa wakazi wa maeneo hayo waliokuwa wanakabiliwa na uhaba wa maji kwa muda mrefu.

Mradi wa maji Nzasa - Somelo ni moja ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na DAWASA kwa lengo la kuondoa changamoto ya maji kwa wananchi walio pembezoni mwa mji na kuboresha hali ya maisha.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Msimamizi wa miradi DAWASA, Mhandisi Aziz Namanga amesema kazi ya upimaji wa wingi wa maji imekamilika kwa asilimia 100 ambapo tayari majaribio yamefanyika kwa kisima kuonyesha uwezo wa kuzalisha lita 200,000 kwa saa. 

“Kazi imefanyika kwa kufanya majaribio ya kuona uwezo wa upatikanaji wa maji katika kisima hiki chenye urefu wa mita 204 na kimeonyesha uwezo wa kuzalisha maji lita 200,000 kwa muda wa saa moja hivyo kufika lita Milioni 4.8 kwa saa 24," amesema.

Mhandisi Aziz Namanga amesema kisima hicho kitahudumia wakazi takribani 68,600 wa maeneo yaliyopo katika kata ya Zingizwa, Msongola na Chanika na kazi iliyobaki ni ulazaji wa mabomba kwa umbali wa kilomita 75.

"Jumla ya wakazi 68,600 watanufaika na huduma ya Maji kupitia kisima hiki ambapo wakazi 12,700 kutoka kata ya Zingizwa, wakazi 27,800 katika kata ya Msongola na wakazi 27,700 katika kata ya Chanika watanufaika na huduma ya Maji," ameongeza.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Zingiziwa, Ndugu Erick Ishengoma amesema hali ya upatikanaji wa maji kwa wananchi sio ya kuridhisha kutokana na kutegemea visima vifupi binafsi ili kupata maji. 

"Niwapongeze DAWASA kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji, matarajio yetu ni kila mwananchi apate huduma ya majisafi kwa ajili ya matumizi," amesema ndugu Ishengoma.

Ndugu Yustina Robert, mkazi wa mtaa wa Ngobedi, kata ya Zingiziwa amepongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo kwani unakwenda kumaliza changamoto ya upatikanaji ya maji ikiwemo kufuata maji kwa umbali mrefu.