Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
WAKAZI 8,939 WA KIDUGALO, KICHANGANI KUNUFAIKA NA MRADI MPYA WA MAJI
25 Apr, 2025
WAKAZI 8,939 WA KIDUGALO, KICHANGANI KUNUFAIKA NA MRADI MPYA WA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekamilisha maboresho ya mradi wa kijamii wa majisafi pamoja na upanuzi wa mtandao wa kulaza mabomba uliochukuliwa na Mamlaka kutoka kwa wanajamii mwaka 2019. 

Akielezea hatua ya utekelezaji wa maboresho ya mradi huu, Msimamizi wa mradi DAWASA Mlandizi Mhandisi Ally Migeyo amesema mradi huu ambao kwa sasa umekamilika, umesanifiwa kuhudumia wakazi takribani 8,939 ambapo mpaka sasa umefanikiwa kuunganisha wananchi 479 katika mfumo wa maji wa Mamlaka na kazi bado inaendelea. 

Ameongeza kuwa wakati mradi unapochukuliwa ulikuwa na uwezo wa kuhudumia wakazi 127 waliokuwa wakichota maji kwenye  Vioski vya Kijamii (Vizimba). 

"Utekelezaji wa mradi umegharimu jumla ya Shilingi milioni 114.9 mpaka kukamilika kwake ili wananchi wanufaike kwa ufanisi," amesema Mhandisi Migeyo.

Amesema kuwa Mradi unanufaisha wakazi wa maeneo ya Kidugalo, Kichangani sehemu ya Mihande na Athena. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Shabani Mchora amesema kuwa maboresho ya mradi huu ni hatua kubwa katika kutoa huduma iliyo bora na ya ufanisi kwa wananchi. 

Ameeleza kuwa mradi huu kabla ya kuchukuliwa na Mamlaka ulikuwa ukitoa huduma kwa watu wachache, lakini kwa sasa baada ya maboresho ya mradi upatikanaji wa huduma umeimarika na sasaa wakazi wengi wanapata maji kwa uhakika. 

Mnufaika wa mradi Bi Veronica Mgaya amesema kukamilika kwa mradi huu umetusaidia kupata unafuu wa huduma ya maji na kutupunguzia adha ya kwenda mbali. 

"Tunashukuru Serikali kwa kutujali na kutusogezea huduma ya maji karibu na makazi yetu, hii inatuwezesha sisi kutekeleza majukumu mengine kwa utulivu," amesema Bi Victoria.