Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
WAKAZI KIGERO WAPOKEA MATUMAINI MAPYA, MRADI WA MAJI WAFIKIA HATUA ZA MWISHO
22 Oct, 2026
WAKAZI KIGERO WAPOKEA MATUMAINI MAPYA, MRADI WA MAJI WAFIKIA HATUA ZA MWISHO

Mradi wa kusogeza huduma ya maji katika eneo la Kigero Umwa, Kata ya Kongowe, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, unakaribia kukamilika huku ukitoa matumaini makubwa kwa wakazi wa eneo hilo kuondokana na changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi.

Mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa Kihuduma Kibaha, unalenga kuwafikishia huduma ya maji wananchi wapatao 580 ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji.

Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, Mhandisi wa Mradi, Ally Migeyo, amesema kazi zinaendelea kwa kasi na mradi umefikia hatua muhimu kuelekea kukamilika.

"Mradi huu unahusisha ulazaji wa mabomba ya inchi tatu kwa umbali wa kilomita mbili. Hadi sasa tayari kilomita 1.8 zimelazwa na kazi inaendelea ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji ndani ya mwezi huu,” amesema Migeyo.

Ameeleza kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa DAWASA wa kusogeza huduma ya maji karibu na wananchi na kufikia malengo ya kitaifa ya upatikanaji wa maji ifikapo mwaka 2030.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigero Umwa, Richard Ngereja, amesema maendeleo ya mradi yameongeza imani kwa wananchi kuwa kero ya maji ipo mbioni kuwa historia.

"Wananchi wetu wameusubiri mradi huu kwa muda mrefu. Hatua iliyofikiwa sasa inaonyesha kweli mradi uko mbioni kukamilika na matumaini yetu ni kuona maji yakianza kutoka kwenye makazi yetu,” amesema Ngereja.

Naye mkazi wa Kigero Umwa, Rehema Juma, amesema kuwa kukamilika kwa mradi kutaleta nafuu kubwa kwa familia nyingi na kuleta unafuu kwa wanawake na watotoambao wamekuwa  wakibeba mzigo mkubwa wa kutafuta maji

Kukamilika kwa mradi huu  kunatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa maji, kupunguza adha ya kutembea umbali mrefu na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.