Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
WAKAZI KING'S - KIMARA KUONDOKANA NA CHANGAMOTO YA MAJISAFI
23 Oct, 2025
WAKAZI KING'S - KIMARA KUONDOKANA NA CHANGAMOTO YA MAJISAFI

Takribani wakazi 1,200 wa mtaa wa King's, Kata ya Kimara wamehakikishiwa huduma ya majisafi, salama na toshelevu mara baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kutekeleza mradi wa uboreshaji huduma katika mtaa huo.

Mradi wa maji mtaa wa King's -Kimara unakwenda kunufaisha wakazi wa maeneo ya King's, Lami Makopo, pamoja na Makaburini maeneo yanayopatikana Kata ya Kimara, Wilayani Ubungo.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Makongo, Mhandisi Boniphace Philemon amesema umuhimu wa mradi huo kwa wakazi hao na hali ya huduma itakavyokuwa baada ya kukamilika kwake.

"Mtaa huu wa King's ulikuwa unapata maji kwa kiwango kidogo sana na hata kipindi cha mgao muda mwingine maji hayakuwafikia, kukamilika kwake kutafanya wakazi hawa kupata maji kwa siku 5 ndani ya wiki kutoka siku 3 za awali," amesema Mhandisi Boniphace.

Mhandisi Boniphace amesema mradi huu wa maboresho ya huduma unajumuisha uchimbaji na ulazaji wa bomba za inchi 6 na 4 kwa umbali wa Kilomita 2.5 ambapo hadi sasa bomba zimekwishalazwa kwa umbali wa kilomita 1.2 na ifikapo mwanzoni mwa Novemba  2025 mradi huu utakuwa umekamilika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa wa Kilungule B, Ndugu Hilary Dimoso ameishukuru DAWASA kwakutekeleza mradi huu kwani eneo la Kings na maeneo jirani yalipata changamoto kwa kipindi kirefu.

"Huduma hii kwetu inakwenda kuwa mkombozi, tunafurahishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi kwani wakazi wa hapa walishindwa kufanya shughuli zao za kimaendeleo lakini pia kutumia gharama kubwa kununua maji.

Sasa tumepata tumaini na maeneo yote maji yalipokuwa yanasumbua huduma inakwenda kuimarika," amesema Dimoso.