Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
WAKAZI MSAKUZI - MACHIMBO HADI MAKABE WATAFUTIWA SULUHU YA MAJI
11 Sep, 2025
WAKAZI MSAKUZI - MACHIMBO HADI MAKABE WATAFUTIWA SULUHU YA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inatekeleza mradi wa uboreshaji huduma ya maji kwa wakazi wa eneo la Msakuzi - Machimbo hadi Makabe.

Mradi huo umehusisha ulazaji wa bomba za inchi 8, 2 na inchi 1.5 kwa umbali wa kilomita 69.1 utakaonufanisha wakazi takribani 39,462 ili kumaliza tatizo la maji kwa wakazi hao.

Akizungumzia mradi huo, Meneja wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Ubungo, Mhandisi Damson Mponjoli amesema utekelezji wa mradi huo unafanyika  kutokana na maeneo hayo kuwa sugu na huduma ya maji haikuwa imara na kusababisha kuwekeza nguvu zaidi kuutekeleza.

"Msakuzi-Machimbo hadi Makabe ni moja ya maeneo ambayo huduma ya majia ilikuwa na changamoto na kutupelekea sisi kama DAWASA kukaa na kutafuta suluhu ya kuhakikisha huduma inaimarika ndipo tumeanza ulazaji wa bomba hizi ambazo zitaongeza msukumo wa maji," amesemayMhandisi Mponjoli.

Mhandisi Mponjoli amesema kutokana na maeneo hayo kuwa na muinuko ndio imeifanya kuwepo na changamoto ya maji ila kwa sasa tatizo hilo linakwenda kumalizika baada ya kazi hii kukamilika.

"Kukamilika kwa kazi hii kutaboresha huduma ya maji na pia uchumi wa wakazi wa maeneo ya Msakuzi, Machimbo hadi Makabe utaongezeka, maana tunatambua maji ndio kila kitu na sasa adha iliyokuwa mwanzo inaenda kuisha kutokana tuko hatua za mwisho kukamilisha," amesema Mhandisi Mponjoli.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Msakuzi, Ndugu Mariam Miraji Kiuko ameishukuru na kuipongeza DAWASA kwa hatua kubwa iliyochukua ya kuimarisha na kuondoa changamoto ya maji iliyokuwa imedumu kwa muda mrefu.

"Mimi kama kiongozi wa mtaa huu tumekuwa na shida ya maji kwa kipindi kirefu ila kwa siku za mbeleni naona tunakwenda kusahau kabisa tatizo hili.

 Nipende kuishukuru DAWASA kwa niaba ya wananchi wangu kwa kutukumbuka na kutuboreshea huduma maana tulikuwa tunapata shida sana," amesema Ndugu Mariam.

Ndugu Radhia Kassim, mkazi wa Msakuzi Kaskazini ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na DAWASA kwa kuondoa changamoto ya maji ambayo imeitesa sana eneo hilo iliyopelekea hata kuharibu ndoa nyingi za wakazi wa eneo hilo.