WAKAZI MSUMI WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA YA HUDUMA YA MAJISAFI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imeanza zoezi la kupokea na kuandikisha wateja wapya wa Mtaa wa Msumi, Kata ya Mbezi, Wilaya ya Ubungo wanaotarajia kunufaika na huduma ya majisafi baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa mradi wa maji Msumi.
Akizungumzia zoezi hilo, Kaimu Meneja Mkoa wa Kihuduma DAWASA Ubungo, Mhandisi Alphonce Magoma amesema, zoezi hilo limeanza kufanyika mara moja kutokana na hatua nzuri iliyofikiwa ya utekelezwaji wa mradi wa maji Msumi ukiwa katika hatua za mwisho.
"Tumeanza zoezi la kuandikisha wananchi ambao wanakwenda kunufaika na huduma ya maji baada ya mradi huu kukamilika, hivyo ni matarajio yetu zoezi hili litakwenda vizuri na tunatarajia kupokea wateja wengi watakaofanya maombi ya huduma ya maji" amesema Mhandisi Magoma.
"Mradi wa Msumi unategemewa kunufaisha wakazi 47,500 hivyo napenda kuwasihi wananchi wote wa Msumi kuwasilisha maombi ili mradi utakapoanza kutoa huduma waanze kunufaika," amesema Mhandisi Magoma.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Msumi, Ndugu Jaqueline Juma ameipongeza DAWASA kwa kuchukua hatua ya kuanza kuandikisha wateja mapema litakalosaidia kupunguza wingi wa wateja kuomba huduma kwa kuwa mradi utakapokamilika wananchi wengi watahitaji kupata maji.
"Napenda kuishukuru na kuipongeza DAWASA kwa kazi kubwa kuanzia utekelezaji wa mradi huu wa Msumi pamoja na kuanza hili zoezi la kuandikisha wateja mapema ili mradi utakapozinduliwa tu basi wananchi waanze kupata maji kwa maana shida ya maji ilikuwa kubwa sana," amesema ndugu Jaqueline.
Sanjali na hayo, mkazi wa Msumi, Ndugu Martin Patrick Msafiri ameipongeza DAWASA kwa kuanza zoezi hili, kwa sababu hamu ya kupata huduma ya maji ilikuwa ni kubwa sana kutokana na changamoto ya maji katika eneo hilo ilikuwa sugu na sasa neema na furaha imekaribia baada ya kukamilika kwa mradi.
Mradi wa Maji Msumi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu, na kunufaisha wakazi takribani 47,500 wa Msumi A, Msumi B na Msumi C pamoja na maeneo jirani.
