Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
WAKAZI STAKISHARI WAITWA KUTATULIWA CHANGAMOTO ZA MAJI
30 Sep, 2025
WAKAZI STAKISHARI WAITWA KUTATULIWA CHANGAMOTO ZA MAJI

Mamlaka ya  Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imefungua dawati rasmi la huduma kwa wateja katika ofisi ya Serikali ya mtaa wa Stakishari, kata ya Kipawa katika Wilaya ya Ilala likiwa na lengo la kusikiliza, kutatua na kutoa suluhu ya changamoto za Wateja juu ya huduma za Majisafi.

Afisa huduma kwa wateja DAWASA- Kinyerezi, Linah Kikoti amesema hatua hiyo inalenga kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kutoa majibu kwa changamoto mbalimbali za kihuduma ikiwemo hitilafu kwenye miundombinu, maombi ya maunganisho mapya na nyingine zihusuzo huduma ya maji.

"Dawati hili litakuwa hapa katika ofisi za Serikali ya mtaa Stakishari likiwa na jukumu la kupokea na kushughulikia changamoto za Wateja na pia kutoa elimu mbalimbali za DAWASA kama vile usomaji wa mita ya Maji, Sheria za ulinzi wa Miundombinu ya Maji, jambo linalotarajiwa kurahisisha usimamizi wa huduma."ameeleza ndugu Kikoti

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Stakishari, ndugu Ibrahim Mavura ameishukuru DAWASA kwa hatua hiyo akisema itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kero zinazohusiana na huduma ya maji na kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

"Nitoe  wito kwa DAWASA kuendelea kuboresha huduma zake katika maeneo mengine ya jiji kwa kuwafikia wakazi wengi zaidi" amesema ndugu Mavura.

Mtaa wa stakishari ni miongoni mwa mitaa nufaika ya huduma ya Majisafi kupitia utekelezaji wa mradi wa Maji Bangulo uliotekelezwa katika kata 14 na mitaa 30 katika Majimbo matano ya uchaguzi ambayo ni Ubungo, Segerea, Temeke, Ukonga na Ilala.