Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
WAKAZI, VIWANDA KISARAWE II WABORESHEWA UPATIKANAJI MAJI
07 Aug, 2025
WAKAZI, VIWANDA KISARAWE II WABORESHEWA UPATIKANAJI MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), inafunga pampu mpya ya kusukuma maji katika moja ya kisima kirefu kilichopo kata ya Kisarawe II, Kigamboni ili kuboresha huduma ya maji maeneo ya viwanda na makazi yaliyopo ndani ya kata hiyo.

Zoezi la ufungaji wa pampu mpya unatekelezwa katika kisima namba 11 cha kuzalisha maji chenye urefu wa mita 415.8 na uwezo wa kuzalisha maji lita 450,000 kwa saa.

Maboresho hayo yanakwenda kunufaisha wananchi takribani wa maeneo ya mitaa ya Tumaini, Kichangani, Kigogo pamoja na Viwanda vya Watercom drinking water, Kiwanda cha dawa (Dawason), Sitafill, Medical Dawlia Limited na Megapipe.

Akizungumza wakati wa zoezi la ufungaji wa pampu hiyo, Kaimu Meneja wa Huduma za Visima DAWASA, Mhandisi Francisca Merere amesema kazi ya ufungaji wa pampu kwa hatua ya awali imekamilika kwa maunganisho ya pampu pamoja na mota zilizounganishwa na nyaya za kebo ili kuruhusu misombo (compounds) iweze kuimarika.

"Kwa hatua ya awali, tumekamilisha kuunganisha pampu mpya, kazi nyingine ni kuunganisha nyaya za umeme katika kebo maalum zilizoweka compounds zitakazohitaji kukauka ili ziweze kuwa imara ili kumalizia hatua ya mwisho," amesema Mhandisi Merere.

Mhandisi Merere amesema kukamilika kwa kazi hiyo kutasaidia uboreshwaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa kata ya Kisarawe II pamoja na baadhi ya maeneo ya Ilala.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi wa Maji Kigamboni, Mhandisi Thadei Mwanjombe amesema kazi ya awali imekamilika na kinachofuata ni maunganisho ya pampu katika mtandao wa usambazaji maji ambapo kazi hiyo itafanyika leo na baada ya hapo huduma ya maji itarejea.

"Tumekamilisha kuunganisha pampu na mfumo wa umeme na leo tutakamilisha zoezi kwa kuingiza pampu mpya katika mtandao wa usambazaji maji ili huduma iweze kurejea kwa wananchi wanaohudumiwa na Tenki la Kisarawe II," amesema Mhandisi Mwanjombe.

Anord Philemon, mkazi wa Kisarawe II ameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa kazi hiyo na kuwataka watendaji wa Mamlaka kuongeza nguvu zaidi ili ikamilike kwa wakati na kuleta matokeo chanya kwa jamii.

"Awali tulipata changamoto ya huduma kuwa sio ya kuridhisha, huku baadhi ya maeneo yakipata maji kwa msukumo mdogo sana na mengine kukosa kabisa, ufungaji wa pampu hii tunategemea kuimarisha huduma na kumaliza changamoto zote zilizokuwepo hapo awali," amesema Philemon.