WAKAZI WA MANGA KUUNGANISHIWA HUDUMA YA MAJI KWA MKOPO

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameanza ziara ya siku tano ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya majisafi inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) katika Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga.
Akiongea na wananchi wa Kijiji cha Manga Kata ya Mkata Wilayani Handeni, Mhe. Aweso ameielekeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuwaunganishia wananchi wa maeneo huduma ya majisafi kwa mkataba wa kulipa kwa mkopo.
"Dar es Salaam mliwauganishia wananchi huduma ya majisafi kwa mkataba wa mkopo, sasa kwanini mshindwe huku, hivyo naelekeza hapa Manga muwaunganishie pia wateja ili waanze kunufaika na maji," alisema Mhe. Aweso.
Aidha amewataka wananchi kuhakikisha wanalipa bili zao za maji kwa wakati ili Serikali iweze kuimarisha utoaji wa huduma kwa ubora na kwa ufanisi.
Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema amepokea maelezo hayo na kuahidi kuwa Mamlaka itaweka utaratibu mzuri wa kutekeleza agizo hilo kwa wakazi wa Kijiji cha Manga.