Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
WAKAZI ZAIDI YA 960 BUYUNI - CHANIKA WAIMARISHIWA HUDUMA YA MAJI
09 Oct, 2025
WAKAZI ZAIDI YA 960 BUYUNI - CHANIKA WAIMARISHIWA HUDUMA YA MAJI

Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea na kazi ya uboreshaji wa miundombinu ya mabomba ya maji ili kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wateja zaidi ya 960 waliopo Mtaa wa Buyuni hadi Chanika, Wilaya ya Ilala.

Maboresho hayo yanahusisha kazi ya kuunganisha njia ya ziada ya bomba la maji lenye kipenyo kikubwa cha inchi 8 na 10 kutoka Bomba la Mradi wa Benki ya Dunia na kuingiza katika bomba lililipo sasa la inchi 2 na 4.

Kazi hii ya maboresho ya miundombinu ya maji inatekelezwa na DAWASA Mkoa wa Kihuduma wa Kisarawe inafanyika katika maeneo ya Buyuni Viwanja vya DAWASA, Buyuni Sekondari, Taliani (mtaa wa Kajuna na Mazinda) pamoja na Mgeure Juu – Kigoma One.

Kukamilika kwa maboresho hayo kutaongeza upatikanaji wa maji na kuimarisha huduma kwa wateja 960 wanufaika wa mradi huu, wakiwemo wakazi wa Buyuni, Mgeure Juu, Taliani, Nyeburu na Hospitali ya Chanika Nguvukazi ambao awali walikuwa na changamoto ya kupata maji kidogo kutokana na kupungua kwa msukumo wa maji.