WANAFUNZI MLIMANI WAPEWA ELIMU YA MAZINGIRA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa elimu ya umuhimu wa maji na hatua za uzalishaji maji kwa wanafunzi wa klabu ya mazingira shule ya msingi Mlimani, Wilaya ya Ubungo, mkoani Dar es salaam.
Lengo la elimu ni kuwaelemisha wanafunzi thamani ya maji na umuhimu wake toka yanapozalishwa mpaka kumfikia mtumishi wa mwisho ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa huduma hii muhimu katika jamii.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule hiyo, Afisa Mawasiliano kutoka DAWASA, Bi Prisca Makenya amesema maji ni rasilimali muhimu ambayo inahitajika kwa viumbe hai ikiwepo binadamu, mimea na wanyama, hivyo kuna ulazima wa kuyatunza na kuhakikisha yanalindwa ili yaweze kufaa kwa matumizi ya kila siku.
"Uzalishaji wa maji hadi kumfikia mtumiaji wa mwisho hupitia takribani hatua nane toka yanapovunwa kwenye mto au chanzo hadi pale yanapofikia kusukumwa kwenda kwa mtumiaji.
"Hatua zote hizi, huusisha gharama kubwa kuyaandaa maji hivyo ni vyema tukawa mabalozi wazuri kwa kuthamini kila tone la maji," amesema Bi.Makenya.
Bi. Makenya amesema klabu za mazingira mashuleni zimeanzishwa kwa lengo la kuwajengea vijana uwezo katika masuala ya maji na usafi wa mazingira ili wanafunzi hao wakawe chachu na mabalozi wa mabadiliko kwa jamii wanazotoka na wanafunzi wenzao.
Katika hatua nyingine, wanafunzi wamejifunza njia mbalimbali ambazo jamii inaweza kutumia kulinda vyanzo vya maji kama vile kutofanya shughuli za uharibifu wa mazingira karibu na vyanzo vya maji, kutokata miti ovyo karibu na vyanzo vya maji, kupanda miti na kutokutupa taka ngumu hovyo katika au karibu na vyanzo vya maji.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya msingi Mlimani, Mwanzo Lazaro ameishukuru Mamlaka kwa kutoa elimu hii muhimu kwa wanafunzi wa shule hiyo inayowajengea uelewa wa namma nzuri ya kutunza vyanzo vya maji na jinsi yanavyozalishwa kwa gharama kubwa, amewataka wanafunzi waliopatiwa elimu hiyo kuwa mabalozi wazuri wa huduma za maji katika jamii yao.
Mwanafunzi, Moureen Mgeni aliyepata elimu hiyo, ameishukuru Mamlaka kwa kuwaelimisha na kuwasaidia kujua aina za vyanzo vya maji, hatua za uzalishaji maji na namna bora ya kutumia maji ili kuepuka matumizi mabaya ya maji na kuahidi watakuwa mabalozi wazuri wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira.
Klabu ya Mazingira Shule ya Mlimani ni moja ya klabu 11 za mazingira ambazo Mamlaka inazisimamia katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani ili kuwajengea uwezo wa kutambua shughuli mbalimbali za Mamlaka kuhusu majisafi na usafi wa mazingira na kwenda kuwa mabalozi wazuri katika jamii.
