WANAFUNZI PUGU SEKONDARI WAIPA TANO DAWASA ELIMU YA MAZINGIRA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imefika na kutoa elimu katika klabu ya Majisafi na usafi wa Mazingira katika shule ya Sekondari Pugu iliyopo Wilaya ya Ilala na kusisitiza juu ya umuhimu wa Maji na Usafi wa Mazingira.
Shule hiyo ni miongoni mwa shule 11 za Mazingira zinazosimamiwa na kuendeshwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Afisa Mawasiliano kutoka DAWASA Bi. Hashura Kamugisha ameeleza umuhimu wa usafi wa Mazingira shuleni na maeneo yote yanayotuzunguka, na kusisitiza utunzaji wa sahahi wa taka shuleni katika kuhakikisha shule na mazingira yanakuwa sehemu salama ya kujifunza muda wote.
"Mazingira safi na salama huchochea hali ya kujifinza, mazingira safi yana mchango mkubwa katika kufanya masomo kuwa ya kuvutia zaidi na ni muhimu kwa afya ya akili kwani uepusha magonjwa katika mazingira yetu, hivyo ili kuhakikisha tunaendelea kufurahia mazingira yetu hatuna budi kuyatunza vyema na kujiepusha kutupa taka ovyo na kufuta taratibu zote za usafi zilizopo shuleni" ameeleza Ndugu Kamugisha.
Nae Mwalimu Andrew Cheyo mlezi wa klabu ya mazingira shuleni hapo ameishukuru Mamlaka kwa jitihada za kuwa bega kwa bega na na klabu hiyo shuleni hapo,na kutoa elimu ya umuhimu wa maji, pamoja na suala la usafi wa Mazingira kwa wanafunzi.
"Maji ni muhimu katika jamii kwani hutumika kila siku katika shughuli mbali mbali za binadamu, mazingira bila maji yanaweza kupelekea magonjwa mbalimbali katika jamii,ivyo elimu hii ni muhimu na ni chachu ya kuleta mabadiliko chanya kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla." ameeleza Mwl.Cheyo.
Mwanafunzi Clinton Mayunga ambae ni mwanachama wa klabu ya maji na usafi wa Mazingira ya Shule ya SekondariPugu ameishukuru DAWASA kwa kuwa mlezi na kutoa nafasi ya wao kujifunza mambo mbalimbali ya Maji na Usafi wa Mazingira na kuomba nafasi ya kuendelea kujifunza kwa vitendo ili kufahamu zaidi namna Mamlaka inavyoendesha shughuli zake.
"DAWASA imekuwa mlezi wa klabu yetu ya mazingira kwa muda sasa na kila mara tunajifunza vitu mbalimbali kuhusu Majisafi na Usafi wa Mazingira.Elimu ya leo imesaidia kujenga uelewa zaidi kuhusu matumizi sahihi ya maji hasa kwa sisi wanafunzi ili kuweza kupunguza gharama kubwa ya bili za maji na kuendelea kupata huduma ya maji endelevu.
Mamlaka inasimamia kalabu za mazingira shuleni kwa kutoa elimu mbalimbali kuhusu Majisafi na Usafi wa mazingira, utunzaji wa miundombinu ya maji,utunzaji wa vyanzo vya maji na kuwaandaa wanafunzi katika rika lao kuwa mabalozi wema katika jamii katika masuala yote yanayohusu maji.