Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
WANANCHI 500 WATAFUTIWA SULUHU YA MAJI
14 Aug, 2025
WANANCHI 500 WATAFUTIWA SULUHU YA MAJI

Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imeanza kutekeleza mradi wa kuongeza mtandao wa huduma ya majisafi utakaonufaisha wakazi zaidi ya 500 wa eneo la Mtaa wa Bangulo Mwanapindi, Kata ya Pugu Stesheni, Wilaya ya Ilala.

Mradi huu ni sehemu ya matokeo ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa Usambazaji maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo) uliotekelezwa na DAWASA kwa gharama ya Shilingi Bilioni 36.9 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Akizungumza wakati wa zoezi la uchimbaji mitaro kwa ajili ya ulazaji mabomba ya usambazaji maji, Mhandisi Adam Makindai wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Kinyerezi amesema mradi huo umeanza utekelezaji na unatarajiwa kuondoa changamoto ya upatikanaji maji iliyopo katika mtaa huo wa Mwanapindi.

"Kwasasa tunaendelea na hatua ya uchimbaji mitaro ili kulaza mabomba ya kipenyo cha inchi 1.5", inchi 2 na inchi 3 kwa umbali wa kilomita 12.75 ambapo baada ya kukamilika kwa mradi yatahudumia zaidi ya wakazi 500 na kutatua changamoto ya ukosefu wa majisafi katika eneo la Mwanapindi," amesema Mhandisi Makindai.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bangulo, Kata ya Pugu Stesheni, ndugu Goodluck Mwele ameishukuru DAWASA kwa kuwaletea mradi huu ambao utasaidia kuboresha upatikanaji wa majisafi na salama pamoja na kuboresha hali ya uchumi kwa wakazi wa Bangulo Mwanapindi.

"Eneo hili limekuwa na hali ngumu ya upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa takriban miaka 10 wananchi wanapata maji yasiyo salama kutoka katika Mabwawa au kununua kwa Shilingi 5,000 au zaidi kwa uniti moja lakini ujio wa mradi huu unaleta matumaini ya kupata majisafi na salama na kwa gharama ya kumudu ambayo ni 1,679.63 kwa uniti moja," amesema ndugu Mwele.

Mkazi wa Mwanapindi, ndugu Anna Joseph Lyimo ameishukuru Serikali ya Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na DAWASA kwa kuwaondolea kero ya maji ambayo imewatesa kwa muda mrefu.

"Kwakweli tunapata shida sana ya maji, ni tabu kuyapata na tunanunua kwa gharama kubwa ambayo sio kila mtu anaimudu, mradi huu utatukomboa akina mama na kupunguza gharama za kununua maji," amesema ndugu Anna.