WANANCHI WA MUHEZA, KIBAHA WAPATA AHUENI BAADA YA KUFIKISHIWA HUDUMA YA MAJI
Wananchi zaidi ya 200 wa mtaa wa Muheza, Kata ya Mailimoja, Wilaya ya Kibaha, Mkoani Pwani, wameelezea furaha yao ya kuanza kunufaika na huduma ya majisafi waliyoikosa kwa kipindi kirefu baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kufikisha huduma ya majisafi katika eneo lao.
Akielezea shuhuda mbalimbali kwa niaba ya Wananchi, Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Muheza Ndugu Jackson Msukulu alisema, hii ni hatua muhimu sana kwetu wananchi wa mtaa huu kwa kuwa shida ya maji ilikuwa kubwa sana katika eneo letu na kwa muda mrefu.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa maji ulikuwa mgumu sana, wananchi walikuwa wanatumia maji ya kisima ambayo yalikuwa na chumvi nyingi na kusababisha wananchi kuathirika kiafya kutokana na kiwango kikubwa cha chumvi iliyokwepo kwenye maji.
"Lakini pia, wanawake walikuwa wanafuata maji kwa kutembea umbali mrefu na kuathiri ratiba za shughuli zao mbalimbali, tunaishukuru sana DAWASA kwa kufanikisha kusogeza huduma katika maeneo yetu, kwa kuwa imeleta matumaini, furaha na kutusaidia kupata muda wa kufanya kazi nyingine," ameeleza Ndugu Msukulu.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huu Bi Catherine Minja ameishukuru Serikali kupitia Mamlaka kwa kuona shida waliyoipitia kwa muda mrefu ya kukosa maji na kuwa kuwahudumia.
"Tumefarijika sana kwa kupata maji katika maeneo yetu, maana tulipata tabu kwa muda mrefu, tunaishukuru DAWASA kwa jitihada hizi, ambazo zimesaidia kuokoa afya zetu, ma kuboresha ustawi wa familia zetu," amesema Bi Catherine.
Kwa upande wake Msimamizi wa mradi DAWASA Mlandizi Mhandisi Bertha Ambangile amesema kuwa kazi iliyofanyika ilihusisha kutoa toleo kwenye bomba la 24 kwenda kwenye bomba la inchi 6, 3, 2 na 1 ili kufikisha huduma kwa wananchi wote, kuwaondolea adha ya kupata maji na kutimiza haki yao ya msingi ya kupata huduma ya maji ambayo Serikali imewekeza fedha.
Shida ya maji katika eneo hili iliwaathiri takribani wananchi 300 wa mtaa wa Muheza. Na hivyo, kazi ya usambazaji maji tuliyoitekeleza hapa inawezesha wananchi zaidi ya 200 kuanza kupata huduma ya majisafi.
