WATEJA 228 WAANZA KUNUFAIKA NA HUDUMA YA MAJISAFI MLANDIZI
Takribani wakazi 228 wa Kata za Kawawa, Mtongani, Misugusugu na Visiga wamefurahia kupata huduma ya majisafi kutoka Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira (DAWASA) kupitia Mkoa wa Kihuduma Mlandizi.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa lengo la Serikali la kufikisha huduma ya majisafi kwa wananchi wote.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo lililofanyika kipindi cha mwezi Oktoba, Mhandisi Ally Migeyo amesema sambamba na kazi ya kuwaunganisha wateja hao, Mamlaka imekuwa ikitoa elimu kuhusu namna nzuri ya matumizi ya maji majumbani kwa lengo la kuzuia upotevu wa maji na kuepuka gharama kubwa inayotokana na matumizi holela ya maji.
Pia, amesisitiza wananchi kuwa sehemu ya juhudi za kuzuia upotevu wa maji kwa kuripoti miundombinu iliyoharibika na kuhakikisha wanaitunza ipasavyo.
"Tunawahamasisha wananchi kuwa mabalozi wa maji safi katika jamii zao lakini pia kutoa taarifa za uvujaji wa maji au uharibifu wa miundombinu ili kuzidi kuweka mazingira yetu katika hali ya usafi," amesema Mhandisi Migeyo.
Mkazi wa Mtaa wa Jonungh'a, Ndugu Japhet Lukumay amefurahishwa na huduma hii ya maunganisho mpya kwani yamefanyika kwa wakati sahihi tofauti na alivyokuwa akifikiria.
“Nilipeleka maombi ya huduma ya maji mwanzoni mwa mwezi oktoba cha kustaajabisha ndani ya mwezi huohuo nikapata huduma ya maji jambo ambalo sikutegemea, niwaombe muendelee kufanya kazi kwa bidii ili kila mwananchi anufaike na huduma hii muhimu ya maji,” amesema Ndugu Lukumay.
Wateja pia wamekumbushwa juu ya umuhimu wa kuwa na mawasiliano ya karibu na Mamlaka kwa lengo la kupata taarifa na ufafanuzi wa mambo mbalimbali yahusuyo huduma pindi watakapohitaji msaada wowote kutoka DAWASA.
Kwa mawasiliano ya DAWASA Mlandizi wateja wameaswa kutumia namba 0734 130 133 au 181 Bure.
