Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
WATEJA 300 KUUNGANISHWA HUDUMA YA MAJI MLANDIZI
10 Sep, 2025
WATEJA 300 KUUNGANISHWA HUDUMA YA MAJI MLANDIZI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) 
imesema, ndani ya mwezi huu wa Septemba, zaidi ya wateja 300 wa Kata za Vigwaza, Janga, Mtongani na Kawawa wataunganishiwa huduma ya maji.

Hatua hiyo ya uunganisha maji unaofanywa na DAWASA, Mkoa wa Kihuduma Mlandizi ni kuendelea kutimiza malengo ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwa zaidi ya asilimia 85.

Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji vifaa vya maunganisho,
Mhandisi Ally Migeyo amesema ni sehemu ya mkakati wa Mamlaka kuhakikisha kila mkazi wa Mlandizi anaunganishwa na huduma ya maji safi ili kuboresha afya na ustawi wa jamii katika maeneo mbalimbali hasa yanayoendela kukua kwa kasi kama Mlandizi.

“Huduma ya maji ni haki ya msingi kwa kila mwananchi na uunganishaji huu, umewekwa kama sehemu ya mkakati wa Mamlaka wa kupanua wigo wa huduma zake pamoja na  kuimarisha miundombinu ya upatikanaji wa maji safi kwa jamii bila usumbufu wa kutembea umbali mrefu au kutegemea vyanzo visivyo salama,” amesema Mhandisi huyo.

Mkazi wa Kijiji cha Mnindi, Ndugu Swaum Ramadhan ameishukuru DAWASA kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji, hii imeleta faraja sana faraja kubwa kwani  adha ya kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kushughulikia shughuli za maendeleo, imekwisha 

“Hatua ya kuletewa vifaa vya maunganisho ya huduma katika maeneo yetu, ni faraja sana kwetu, kwani imeokoa muda kwa kupata huduma hii ndani ya muda mfupi kutasaidia hata kuboresha shughuli za kiuchumi, ikiwemo biashara ndogo ndogo zinazohitaji maji ya uhakika," amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnindi Ndugu Juma Chambwewe amesema furaha yake kuona DAWASA wamewafuata majumbani kwao ili tu kuhakikisha kwamba kila mwananchi anapata huduma ya maji kwa wakati na kwa muda mfupi.

“Jambo hili la kuwaletea wananchi vifaa vya maunganisho majumbani, na kuhakikisha kila aliyeomba huduma amenufaika ni jambo la baraka sana, tunawashukuru sana na kuwapongeza katika utumishi wenu," amesema Ndugu Chambewe.