Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
WAZIRI AWESO AKAGUA HUDUMA YA MAJI DAR ES SALAAM, AWAPA MAAGIZO WANANCHI, DAWASA
08 Dec, 2025
WAZIRI AWESO AKAGUA HUDUMA YA MAJI DAR ES SALAAM, AWAPA MAAGIZO WANANCHI, DAWASA

Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mb) ametembelea na kukagua huduma ya maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na kukagua hali ya uzalishaji maji katika mtambo wa maji Ruvu Chini Wilayani Bagamoyo.

Ni baada ya kuwepo kwa upungufu wa huduma ya maji iliyosababishwa na kupungua kwa wingi wa maji katika mto Ruvu kufuatia mabadiliko ya tabia ya nchi, kuongezeka kwa joto pamoja na kuchelewa kwa mvua.

Mheshimiwa Aweso ametumia nafasi hiyo kutoa maelekezo kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ili kuhakikisha maji haya yanayozalishwa kwasasa yanafikia wananchi wote kwa usawa na kutoleta taharuki kwani kipindi hiki ni cha mpito na hali itarejea vizuri.

"Ni kweli uzalishaji wa maji umepungua, lakini bado maeneo mengi yanapata maji, nimepita maeneo ya tenki la Kimara, Ubungo, Mabwepande, hadi Mbweni wananchi wanapata huduma ya maji, nitoe rai kwa wananchi kutumia maji haya kwa uangalifu na kuhifadhi zaidi ili yaweze kuwasaidia na wale ambao bado hawatapata huduma niwahakikishie wote watafikiwa," amesema Mheshimiwa Aweso.

Aweso ameongeza kwa kuagiza visima vyote vilivyochimbwa na Serikali kuunganishwa katika mfumo wa DAWASA ili kuongeza wingi wa maji na kuhakikisha kazi hii inakua shirikishi kwa raasisi binafsi na mashirika ya dini yenye umiliki wa visima ili kusaidiana kuwapatia wananchi huduma ya maji.

Kwa upande mwingine Mheshimiwa Aweso ameagiza kusitishwa kwa shughuli nyingine zinazotumia maji kutoka mto Ruvu na badala yake maji hayo kwasasa yabaki kwa matumizi ya binadamu pekee mpaka pale mvua zitakaponyesha na hali kuwa sawa.

Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, MheshiwaAlbert Msando amesema ofisi yake itakua mstari wa mbele kusimamia maji haya yanayopatikana kwasasa yanamfikia kila mwananchi kwa usawa na kushughulika na tatizo la upotevu wa maji.

"Zaidi na hilo hatutaruhusu watoa huduma binafsi wenye kibali cha kuuza maji toka DAWASA wageuze changamoto hii kuwa fursa na kuwauzia wananchi maji kwa bei kubwa ya ulanguzi, hilo hatutakubaliana nalo," amesema Mheshimiwa Msando.

Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi DAWASA, Mhandisi Romanus Mwang'ingo amesema kwaniaba ya uongozi wa DAWASA wamepokea vyema maagizo ya Waziri wa Maji na Mamlaka haitalala bali kufanya kazi usiku na mchana ili kila mwananchi apate huduma.