WAZIRI AWESO APONGEZA USHIRIKIANO WA DAWASA, WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA

Waziri wa Maji, Mhe Jumaa Aweso amesema ushirikiano baina ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa utawafanya kuwa mabalozi na walinzi kwa huduma za majisafi.
Waziri Aweso ameyasema haya leo Jumanne, Februari 18, 2025 katika kikao kazi cha DAWASA na Wenyeviti wa Serikali za mitaa akieleza kuna changamoto zingine zinatatuliwa na Wenyeviti wa Serikali za mitaa, hivyo kuwashirikisha ni kuboresha huduma ya maji.
"Niwasihi sana haya mashirikiano yakiboreshwa zaidi yatachangia kwa kiasi kikubwa kutoa ulinzi wa huduma ya maji, kwani Viongozi hao watalinda huduma hiyo kwa wivu mkubwa," amesema Waziri Aweso.
Pia amewapongeza DAWASA kwa kusimamia ipasavyo mradi wa maji Bangulo akieleza kuwa mradi utasaidia zaidi kuongeza upatikanaji wa maji katika maeneo mengi hasa ya Kinyerezi, Tabata na maeneo mengi zaidi.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule usambazaji wa maji katika Wilaya ya Kinondoni kwa sasa umefikia asilimia 97 na hii ni kwa sababu usiku na mchana watendaji wa DAWASA wamekuwa wakihakikisha kuwa wanafuatilia na kusambaza maji katika kila Kata na Vitongoji.
"Niwajibu wetu sisi wananchi wa Kinondoni kuilinda DAWASA kwa wivu mkubwa, kwani huduma wanayotupatia ni muhimu sana kwetu, maji yakikosekana kila jambo linaweza kusimama, hivyo mashirikiano haya," amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema kuboreka kwa mashirikiano kati ya Mamlaka na Wenyeviti wa Serikali za mitaa kutatatua changamoto mbalimbali kwani zingine zisizofikiwa na DAWASA zitatolewa taarifa kupitia viongozi hao.
Kaimu Mtendaji Bwire amemshukuru Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya kusambaza maji katika jiji la Dar es Salaam kwani hivi sasa DAWASA wanatekeleza miradi mikubwa ya kuhakikisha kuwa wastani wa upatikanaji wa maji unaongezeka kwa kasi kila siku.