Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
WAZIRI AWESO ARIDHISHWA NA JITIHADA ZA UBORESHAJI HUDUMA YA MAJI DAR, PWANI
30 Oct, 2024
WAZIRI AWESO ARIDHISHWA NA JITIHADA ZA UBORESHAJI HUDUMA YA MAJI DAR, PWANI

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso(Mb) ameipongeza Wizara ya Maji na timu ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kuungana na kutatua changamoto za huduma ya maji kwenye maeneo mengi hususani wananchi wanaohudumiwa na Mtambo wa kuzalisha maji Ruvu Juu ikiwemo maeneo ya Kinyerezi, Bonyokwa, Tabata, Msakuzi na Segerea.

Katika ziara yake ya kutembelea na kukagua upatikanaji wa huduma ya maji kupitia Mtambo wa Ruvu Juu na kuridhika na kiwango cha maji kilichopo pamoja na maboresho ya mfumo wa Maji yaliyofanyika kufuatilia hitilafu iliyotokea hivi karibuni. 

Ameongeza kuwa pamekuwa na malalamiko ya uhaba wa huduma kwenye maeneo ya Kwembe, Msakuzi, Kinyerezi, Bonyokwa na Tabata, lakini kwa sasa huduma ya maji imeimarika na inaendelea kuwa bora zaidi. 

Ameitaka DAWASA kuendelea na kazi ya kufuatilia upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi mara baada ya kukamilika kwa matengenezo ya hitilafu iliyotokea kwenye Mtambo.

"Niwatake viongozi wote wa DAWASA muendelee na zoezi la kufuatilia hali ya usambazaji maji kwa wananchi hususani kwenye maeneo ya Kinyerezi, Tabata, Bonyokwa, Msakuzi na maeneo mengine ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji," ameeleza Mhe. Aweso. 

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa Mamlaka imekamilisha matengenezo ya hitilafu ya umeme iliyotokea kwenye Mtambo wa Ruvu Juu kwa kushirikiana na Shirika la Umeme (Tanesco) na kuwezesha kuimarika kwa huduma ya majisafi kwa wananchi wa maeneo yaliyokuwa na shida. 

Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi Tawala Mkoa wa Pwani Ndugu David Mramba ameishukuru Serikali kupitia Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye sekta ya maji kwa lengo la kumtua Mama ndoo kichwani. 

Amesema kuwa mkakati huu umesaidia kwa kiasi kikubwa kwa wananchi kupata huduma ya maji kwa uhakika.