Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
WAZIRI MKUU MAJALIWA AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA BWAWA LA KIDUNDA
06 Mar, 2025
WAZIRI MKUU MAJALIWA AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA BWAWA LA KIDUNDA

Aagiza Tarafa ya Ngerengere kupata huduma ya Maji

Katika kuadhimisha na kufungua rasmi wiki ya maji, Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa Kassim (Mb) amekagua na kuweka Jiwe la Msingi katika Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kidunda huku akiagiza mradi huu kwenda kunufaisha Kata na Vijiji vyote vinavyozunguka Mradi kwa kuwapatia huduma ya maji safi na salama.

"Mradi huu ulikuwa ndoto kubwa ya Mhasisi wa Taifa letu, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Tunamshukuru sana Rais wa awamu ya sita Mh.Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za kutekeleza mradi huu muhimu sana" ameeleza Mh. Majaliwa.

Majaliwa ameongeza kwa kuiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha Vijiji vyote vinavyozunguka Mradi huu kupatiwa huduma ya majisafi na salama ili waweze kuona manufaa ya uwepo wa mradi huu.

Naye Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Awesu (Mb) akizungumza wakati wa hafla hiyo ya uwekaji Jiwe la Msingi ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kufika haraka katika Tarafa ya Ngerengere ili kupata ufumbuzi wa changamoto ya maji katika eneo hilo,

"Maelekezo ya Mheshimiwa Rais katika kila miradi ni lazima wananchi wanaozunguka eneo la Mradi wanufaike na huduma za mradi husika. Ukiwa karibu na Waridi lazima unukie hivyo natoa maelekezo kwa DAWASA kufika Ngerengere wiki hii ili kuona namna ya kuwapatia maji wananchi wakati tunasubiri mradi kukamilika waendelee kunufaika." Amesema Mhe. Aweso.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amewahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma ya maji katika vijiji vinne vya Kata ya Mkulazi, Wilaya ya Morogoro Vijijini vinavyozungukwa na Mradi huo.

"Wizara pia imejipanga kufikisha huduma ya majisafi kwenye Vijiji vinavyozunguka Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kidunda hususan Vijiji vinne kwenye Kata ya Mkulazi ambavyo ni Usungura, Kidunda, Chanyumbu na Mkulazi." Amesema Mhandisi Mwajuma.

"Mradi huu kwa sasa utekelezaji umefikia asilimia 28 na upo katika hatua ya usanifu ambapo ukikamilika utanufaisha wananchi wapatao 7,296," Ameongeza Mhandisi Mwajuma.

Mradi wa Ujenzi Bwawa la Maji la Kidunda umewekwa Jiwe la Msingi na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Kassim na unatekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia fedha za ndani na unalenga kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa muda wote katika Mto Ruvu na kuweka uhakika wa maji katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na Mikoa ya Morogoro na Pwani.